MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amezua tafrani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya askari polisi waliomleta awali kutaka apande gari kwenda mahabusu kwa sababu ya kutokidhi masharti ya dhamana.

Awali, Lema alisomewa makosa mawili yaliyokuwa yakimkabili mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Desdery Kamugisha na Wakili wa Serikali, Innocent Njau.
Katika mashtaka ya kwanza ni la kutuma ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwake kwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Mashtaka ya pili, kutumia Whatsapp kwa ajili ya kuwashawishi wananchi wa Jiji la Arusha, kuandamana Septemba mosi.
Baada ya Lema kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Kamugisha alimuuliza kama ni kweli au la; na Lema alikana. Baada ya kukana, wakili Njau aliomba Lema asipewe dhamana kwa sababu wana taarifa za kiintelijensia kuwa endapo atapewa dhamana, usalama wake utakuwa mashakani.
Hoja ya wakili huyo wa serikali, ilipingwa na wakili wa utetezi, John Mallya. Baada ya mabishano hayo, Hakimu Kamugisha alitupilia mbali pingamizi la wakili Njau la Lema kunyimwa dhamana.

Baada ya sharti la dhamana kutolewa, wadhamini wawili walijitokeza ambao ni madiwani wa Jiji la Arusha. Lakini, hali tofauti ilijitokeza baada ya wakili wa serikali, Njau kukagua barua ya kumdhamini Lema na kugundua kuna kasoro za matumizi ya majina.
Kutokana na sintofahamu hiyo, hakimu alikubaliana na hoja ya wakili Njau na kusema kuwa Lema atafute wadhamini wengine na kuahirisha kesi hiyo kwa muda hadi Septemba 19 mwaka huu.
Baada ya kusomewa kesi hiyo, ikasomwa kesi ya pili ambayo inadaiwa ya kutoa lugha ya uchochezi kati ya Agosi mosi hadi 26 mwaka huu kwa njia ya kurekodi kwa sauti ‘audio clip’ na kurusha kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuhamasisha maandamano Septemba mosi mwaka huu.
Saa 8:20 mchana askari polisi walimtoa chumba cha mahabusu na kutaka kumpandisha gari la Polisi kwa ajili ya kumpeleka mahabusu Kisongo. Kutokana na sintofahamu hiyo, Lema alibishana na polisi hao, huku akiwa na mawakili wake, Mallya na James Lyatuu, waliohoji kuwa wanampeleka wapi wakati muda wa mahakama haujafika.
“muda wa mahakama haujafika mnanipeleka wapi, nasema nitafia hapa mahakamani, saa hizi ni saa 8:00 muda wa mahakama haujaisha, mnanipeleka wapi, siendi, mniue, siendi popote, mniue hapa hapa, muda wa mahakama haujaisha, ‘broo’ mnanipeleka wapi na kwa nini mnanifanyia hivi, nasema siendi kokote, bora kufa, sikubali" alisema Lema.