Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
RAIA wa China, Li Xi Uyiang (30) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na pete iliyotengenezwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 32.

Alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Hellen Moshi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
Wakili Moshi alidai mshitakiwa huyo ambaye ni mhandisi anakabiliwa na mashitaka ya kukutwa na nyara za Serikali, analodaiwa kulifanya Agosti 6, mwaka huu katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Inadaiwa alikutwa na pete hiyo iliyotengenezwa kwa kutumia meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 32 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Baada ya kusomewa mashitaka, Hakimu Mkeha alisema mshitakiwa haruhusiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo isipokuwa Mahakama Kuu.
Wakili, Moshi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba apangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 18, mwaka huu.