Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
SERIKALI imelifungia gazeti la Mseto kwa miezi 36 kwa madai ya kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na uongo, zisizozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema amri ya kulifungia gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Namba 242 lililotolewa Agosti 10, mwaka huu.

Nape alisema uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 Sura ya 229, Kifungu 25(1) ambacho kinasema “Waziri akiona kwamba kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya kudumisha amani na usalama inafaa afanye hivyo aweza kutoa amri na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litakoma kutolewa tangu siku itakayotajwa katika amri hiyo.”
Alisema uamuzi huo unazuia gazeti la Mseto kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwamo mitandao kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Sura ya 306.
“Hatua ya kulifungia gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Septemba, 2012 kabla sijawa Waziri hadi Agosti, 2016 kumtaka mhariri wa gazeti kuacha kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari bila mafanikio,” alisema Waziri Nape.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, serikali imelazimika kuchukua uamuzi huo kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za serikali kwa nia ya kumchafua Rais John Magufuli na viongozi wa serikali, lengo likiwa kutaka kumchonganisha na wananchi waliokuwa na matarajio makubwa kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Alisema pamoja na makosa mengine, hivi karibuni gazeti hilo katika toleo namba 480 la Agosti 4-10, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua ya kughushi kutoka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) yenye kichwa cha habari kisemacho “Waziri amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.
“Kwa mujibu wa vyombo vya uchunguzi vya serikali, imebainika kwamba nyaraka hiyo imeghushiwa na wahariri na walipotakiwa kuleta uthibitisho wa nyaraka waliotumia katika gazeti lao, walishindwa,” alisema Nape na kutoa mwito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, ambayo ikizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote.
Alisema serikali inasisitiza kuwa inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na sheria za nchi na kwamba inaahidi kushirikiana navyo.
Alieleza kuwa Serikali imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayoainisha uhuru na mipaka ya habari kama vile Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu 1981.