MAPEMA mwezi Juni, mkongwe kwenye gemu la Muziki Bongo, ambaye pia ni staa wa Wimbo wa Bado Nipo Nipo, Hamisi Mwinjuma aliuaga ukapera baada ya kufunga ndoa na mzazi mwenzake ambaye ni akauntanti, aliyezaa naye mtoto aitwaye Maleka.
Ni zaidi ya miezi miwili sasa mkali huyo akiwa kwenye maisha ya ndoa ambapo akichonga na gazeti hili MwanaFA amefunguka mambo matatu ambayo hayafanyi tangu ‘avute jiko.’ Msikie mwenyewe;

Kupiga Misele sana: “Kwa kweli tangu nioe, imenibidi kupunguza baadhi ya ratiba ambazo zilikuwa zinanichukulia ‘time’ huko nyuma na kunifanya wakati mwingine kuwa nje ya nyumbani. Kwa kuwa mimi siyo mtu wa kujirusha kiivo, suala hili limekuwa rahisi na inanipasa kuwa karibu zaidi na familia.
Kuondoa mtazamo hasi juu ya ndoa. “Kipindi cha nyuma nilikuwa ‘sometime’ nasikia kuwa mtu akioa hasa msanii kuna uwezekano mkubwa wa kupotea kwenye gemu, si kweli, mtazamo huo tangu nioe nimeuondoa kabisa kwa kuwa mke wangu ni mtu wa burudani na anafahamu ninachokifanya. Kikubwa ni kupanga ratiba juu ya mambo yangu na kujua nini natakiwa nifanye katika wakati husika.”
Kujisahau. “ Kuna wakati unafika ukiwa mwenyewe tena mwenye mafanikio unaweza kujisahau na kuona kuwa umefika, mafanikio uliyoyapata yanatosha. Lakini ukweli ni kwamba kutokana na kuwa na familia inanibidi kufanya kazi kwa bidii, kwa kuwekeza kwenye muziki wangu na mambo mengine ili kuhakikisha familia yangu inapata kila kitu inachokitaka. Zaidi ni kuwaandalia maisha bora ya leo na kesho!”
Mbali na hayo MwanaFA alimaliza kwa kuwashauri wanamuziki ambao wanayaogopa maisha ya ndoa na kuamini wakifanya hivyo watafeli kuondoa mtazamo huo na kuwahakikishia kuwa familia ni jambo la heri na humfanya mtu kukomaa zaidi ili kufika mbali