RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amewataka wananchi wa Pemba wasibabaishwe na wanasiasa waliofilisika, wanaowadanganya watu na kusisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu umekwisha na hautafanyika mwingine hadi mwaka 2020 na Ali Mohamed Shein ndiye Rais halali wa Zanzibar.

Amewakemea wanasiasa wanaopita kila kona na wakitembea Ulaya, akisema safari zao hizo zitaishia vichochoroni kwani Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk Shein.
“Nataka niwaambie hao wanaokwenda nje na kujitangaza kwa kujitapa, kwamba Rais aliyepo madarakani kwa sasa ni Dk Shein......uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo mwaka 2020,” alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa kwa nguvu na umati mkubwa wa wananchi.
Rais Magufuli alisema hayo wakati akihutubia umati wa wananchi wa mikoa miwili ya kisiwa cha Pemba, ya Kaskazini Pemba na Kusini Pemba katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale mjini hapa, uliokuwa na lengo la kutoa shukrani wa wananchi wa Pemba kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.
Alisema anakerwa na matukio ya vitendo vya chuki na uhasama ikiwemo watu kuchomeana mali zao ikiwemo mikarafuu, neema ambayo wananchi wamepewa na Mungu.
Alisema matukio hayo yanafanywa kwa lengo la kujenga chuki na uhasama huku baadhi ya watu wakiathirika vibaya baada ya kuharibiwa mazao yao.
Aliongeza kuwa kwamba, wakati akila kiapo cha utii na uaminifu aliahidi kulinda Muungano pamoja na amani na utulivu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kuwaonya viongozi wanaopandikiza chuki na uhasama kwamba atapambana nao kwa nguvu zote kwani hakuna uwekezaji katika nchi iliyojaa vurugu.
Aliviagiza vyombo vya ulinzi kuhakikisha vinawasaka watu wote wanaofanya vurugu kiasi kuhatarisha amani na utulivu.
“Mimi nawashangaa sana watu wa Pemba sijui mnataka nini tena.....mnaye Rais mpole sana ambaye anatoka Pemba sasa sijui mnataka nini jamani,” alihoji Rais Magufuli.
Aliwataka wananchi wa Pemba kutoa ushirikiano wa dhati kwa Rais Shein na kuacha kuwasikiliza wanasiasa waliofilisika ambao kila siku kazi yao kuwadanganya wananchi huku wengine wakijidai wanatoka Ulaya kumbe wapo jijini Dar es Salaam wamejifungia.
“Mimi namfahamu sana Rais Shein....nilifanya kazi naye mimi tangu nikiwa naibu waziri wa uvuvi.....huyu uwezo wake ni mkubwa na itumieni hazina yake,” alisema.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kutoa ushirikiano wa dhati kwa ajili ya kuleta maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda mbalimbali ambavyo vitasaidia kuzalisha ajira.
Kwa mfano, alisema kisiwa cha Pemba kina utajiri mkubwa wa sekta ya uvuvi ambayo ikitumika vyema itasaidia kuimarisha ajira kwa vijana.
Alisema amedhamiria kushirikiana na Rais Shein katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika sekta mbalimbali zikiwemo ujenzi wa viwanda pamoja na utalii.
“Nawaombeni wananchi wa Pemba tufanye kazi pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika kuleta maendeleo....hakuna uchaguzi utakaorudiwa jamani,” alisema Dk Magufuli ambaye ni mara yake ya kwanza kuhutubia hapa, tangu ashinde urais mwaka jana.
Aidha, Rais Magufuli aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kusimamia uchaguzi vizuri ule wa kwanza wa Oktoba 25, mwaka jana wa marudio Machi mwaka huu, huku akimmwagia sifa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.
“Kama kuna mtu anayestahiki kupewa tuzo ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha.....huyu mtu ukipata nafasi ya kutoa tuzo basi umuangalie vizuri sana,”
Dk Magufuli alisema akimueleza Rais Shein. Tangu kumalizika kwa marudio ya Uchaguzi Mkuu Machi mwaka huu, viongozi wa vyama vya upinzani hasa Chama cha Wananchi (CUF) waliosusia uchaguzi huo ambao Dk Shein alishinda kwa kishindo kwa asilimia 91.4, wamekuwa wakipita ndani na nje ya nchi wakidai uchaguzi huo haukuwa halali.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ndiye anayesafiri nje ya nchi akieleza kwenda ‘kuishitaki’ Serikali ya Dk Shein kutokana na malalamiko yao kuhusu uchaguzi huo.