WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga yuko nchini Shelisheli kumwakilisha Rais John Magufuli katika kuongoza ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC) katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika Septemba 8 na 10, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika wizara hiyo, hatua hiyo imekuja baada ya Tanzania kukabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa kuongoza Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC katika Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Mbabane, Swaziland kuanzia Agosti 29 hadi 31, mwaka huu.
Tarifa hiyo ilieleza kuwa wajibu huu wa Tanzania katika kuongoza misheni hiyo ya waangalizi wa uchaguzi imetokana na misingi na mwongozo wa chaguzi za kidemokrasia katika Kanda ya SADC.
Akiwa nchini Shelisheli, Mahiga alizindua rasmi misheni hiyo itakayokuwa na waangalizi kutoka nchi za SADC kwa niaba ya Rais Magufuli.
Aidha, Balozi Mahiga alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa visiwa hivyo, James Michel na pia kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Shelisheli, Joel Morgan na baadaye kukutana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa katika visiwa hivyo.