SERIKALI imetangaza kutoa msaada wa awali wa mabati 20, mifuko mitano ya saruji, mablanketi na mikeka kwa kila muathirika ambaye nyumba yake imebomoka kabisa kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Aidha, wapangaji katika nyumba hizo wametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili wapate mahali pa kujihifadhi.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa anahitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 uliofanyika kwa wiki mbili kuanzia Septemba 6, mwaka huu mjini hapa.
Bunge lijalo litaketi kuanzia Novemba mosi, mwaka huu. Waziri Mkuu pia alitangaza kujengwa kwa miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa, mabweni na vyoo hususani katika Shule za Sekondari za Ihungo na Nyakato zilizofungwa kwa muda wa wiki mbili kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema tathmini za kitaalamu zikikamilika, mpango wa ujenzi wa miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali kwa ajili hiyo.
Katika hotuba yake hiyo ambayo alizungumzia tukio hilo kwa kina, alisema tangu kutokea kwa tetemeko hilo lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha Ritcher 5.7, kwa alasiri ya Jumamosi iliyopita, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na juhudi za kurejesha hali ya utulivu miongoni mwa waathirika.
Katika tetemeko hilo ambalo lilisikika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, liliathiri zaidi mkoa wa Kagera ambako licha ya kusababisha vifo vya watu 17, limejeruhi wengine 253, kuharibu nyumba, vituo vya afya, shule, nyumba za ibada na miundombinu mbalimbali.
Mbali ya kugawa vyakula, kutoa matibabu, Waziri Mkuu alisema serikali imetoa hifadhi za muda za mahema na maturubai kwa wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya makazi kutokana na uharibifu mkubwa uliozikumba nyumba zao.
“Serikali imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Sh milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa. Waziri Mkuu Majaliwa pia alisema serikali imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma, ikiwemo majeshi ya ulinzi na usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa waathirika katika kipindi hiki.
Pia Waziri Mkuu alisema serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalamu kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi. “Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wabunge kwa namna walivyoshirikiana na Serikali kushughulikia janga hilo la kitaifa la tetemeko la ardhi, lakini pia Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kwa kuitikia mwito wa Serikali wa kushiriki na kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeko la ardhi.
Pamoja na kuhimiza wananchi kuendelea kusaidia waliokumbwa na tetemeko hilo, alisisitiza ya kuwa, Serikali itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa, huku akionya watu kutojaribu kujinufaisha binafsi kupitia janga hilo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu jana alipokea msaada wa Sh milioni 121.7 ili kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Msaada huo umetolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni ya Caspian, iliyokabidhi Sh milioni 100 kupitia Meneja Rasilimali Watu wake, Omid Karambech.
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bordar Limited, Wu Yahui aliyetoa Sh milioni 20 na Mariam Kitembe aliyetoa Sh milioni 1.679 kwa niaba ya wauguzi walioshiriki mafunzo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Akipokea msaada huo katika viwanja vya Bunge mjini hapa, Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Kutoka Bukoba, Mwandishi Wetu Angela Sebastian anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu amesema mkoa huo umeunda kamati maalumu kwa ajili ya kugawa misaada iliyokwisha kabidhiwa.
Kijuu alisema hayo jana wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka kwa wadau waliofika mjini Bukoba akiwemo mfanyabiashara Saidi Salim Bakhresa (SSB) ambaye amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 100 ambavyo ni mabati, saruji, mablanketi na magodoro.
Alisema utaratibu umeandaliwa vizuri wa kukabidhi misaada hiyo ambapo hivi sasa kamati hiyo tayari imeanza kujenga mahema kwa baadhi ya wananchi wanaolala nje na kugawa vifaa mbalimbali vilivyopokewa ikiwemo vyakula, mablanketi na magodoro kwa waathirika.
Aliwashauri wananchi kuwa wavumilivu kwani misaada itamfikia kila mmoja na kwamba hakuna ujanja wowote utakaofanyika huku akisema makundi maalum kama wazee, walemavu, wajane na waliopoteza makazi kabisa watapewa kipaumbele.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameitisha harambee kwa wadau mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, taasisi na mashirika mbalimbali ambapo wamechangia kiasi cha Sh milioni 14 taslimu na ahadi Sh milioni 700.
Naye Lucy Ngowi anaripoti kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimepeleka wataalamu wa majengo, umeme, matetemeko na saikolojia mkoani Kagera kwa ajili ya kufanya tathmini ya kutoa ushauri na wa kitaalamu kwa wananchi waliokumbwa na majanga ya matetemeko.
Ofisa Habari chuoni hapo, Jackson Isdory alisema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu mchango wa chuo hicho kwa wananchi walioathirika na tetemeko hilo. Alisema wataalamu hao baadhi yao wameshaondoka na wengine wanaondoka leo kuelekea mkoani Kagera, na itakapoonekana waliokwenda hawatatosheleza, wataalamu wengine watakwenda.