Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa atasimamia kwa nguvu zote masuala yote yanayohusu maendeleo, kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na kudumisha amani kwa faida ya wananchi.
Rais Magufuli amesema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Zanzibar katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kibandamaiti Mjini Unguja.

Dkt. Magufuli ambaye aliongozana na Mkewe Janeth Magufuli amesema ili mambo hayo yafanikiwe Wananchi wa Zanzibar hawana budi kukataa kujihusisha na vitendo vya vurugu na kuvunja amani na amewaonya watu wanaochochea vitendo hivyo kuacha mara moja.
Amewataka wananchi wa Zanzibar kujihadhari dhidi ya wanasiasa ambao wanapandikiza chuki, ubaguzi na fitina, kwani watu hao wanataka kubomoa misingi mizuri ya umoja, upendo na mshikamano wa Taifa uliojengwa na waasisi wa Taifa hili.
Rais Magufuli amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aliyehudhuria mkutano huo, kwa hatua mbalimbali anazozichukua kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar huku akibainisha kuwa tatizo la maji linalovikabili visiwa vya Zanzibar litakwisha baada ya kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa maji utakaofadhiliwa na Serikali ya India kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 92, na mradi mwingine utakaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya Dola za Marekani Milioni 21.
Aidha, Rais Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri vinayofanya katika kusimamia amani visiwani humo huku akivihakikishia kuwa yeye akiwa kiongozi wao anawaunga mkono.Pamoja na Rais Shein Mkutano huo umehudhuriwa na Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume, Mawaziri na Viongozi wa Siasa na wa Dini.