MKUU wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi amekipigia debe Kiswahili na kusema wako gizani wale wanaoamini hakiwezi kutumika kufundishia shule za awali hadi Chuo Kikuu.
Ameyasema hayo kwenye kongamano la Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA) lililofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Iringa, mjini Iringa.

Dk Nchimbi amesema inashangaza kuona wanaotoa kauli hizo ni Watanzania ambao katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku wamekuwa wakiitumia lugha hiyo pamoja na kwamba asilimia kubwa ya lugha waliyotumia kujifunzia ni Kingereza.
“Binafsi nafahamu Kingereza lakini napotumia Kiswahili najiamini na kufanya majukumu yangu kwa uhakika zaidi,” alisema.
Alisema matumizi ya “Kiswanglish na kingereza kibovu” kwa watu wanaoijua lugha hiyo vyema ni kudanganyana na ndio sababu imekuwa ikileta shida hata katika baadhi ya mikataba inayoingiwa na makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Amesema alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 1980, alishuhudia vitabu vya kujifunzia vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili na akahoji sababu ya vitabu hivyo kutotumika hadi sasa.
Alisema kuna haja kwa Watanzania kuienzi lugha yao ya Kiswahili ili wawe na uelewa wa pamoja, na waende na kufika pamoja katika safari yao ya maendeleo.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa, Profesa Joshua Madumulla alisema katika kongamano hilo kwamba Watanzania wanaodhani wanajua Kingereza, wanajidanganya na kama wanataka majibu wanaweza kuyapata kupitia vitabu vilivyoandikwa na Shabani Robert.
Katika kukienzi Kiswahili, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kukuza na kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili.
“Nafurahi kuwafahamisha kwamba serikali imeanza rasmi mchakato wa kuandaa Sera ya Lugha ambayo itatoa mwongozo kwa Taifa kuhusu masuala yote ya lugha ya Kiswahili, lugha za asili, alama, nukta nundu na lugha za kigeni,” amesema.
Wambura alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imekamilisha uanzishwaji wa kamisheni ya Kiswahili ya jumuiya hiyo, ambayo makao yake makuu yapo Visiwani Zanzibar.
“Lengo la uanzishwaji wa kamisheni hiyo ni kukuza na kuendeleza matumizi ya lugha hiyo katika jumuiya hii na duniani kwa ujumla,” alisema na kuongeza kwamba kwa sasa lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi katika jumuiya hiyo na Umoja wa Afrika.