RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kuzingatia yaliyoelezwa kwenye hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli ikiwemo ulinzi wa amani na utulivu nchi.
Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli ameeleza mikakati na malengo ya Serikali zote mbili katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Akitoa hotuba wakati wa Baraza la Iddi kwenye majengo ya Chuo Kikuu cha Mkanyageni Pemba, Dk Shein amesema, Serikali zote mbili zimejizatiti kuhakikisha amani ya nchi inalindwa.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha inatekeleza programu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ili kuleta maendeleo.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha malengo ya mipango ya maendeleo yanafikiwa na kunufaisha wananchi,” amesema.
“Wananchi wa Pemba huu ni wakati wa kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali zote mbili kwa ajili ya kuleta maendeleo. Hotuba ya Rais Magufuli iliyotokana na ziara yake ya siku mbili Unguja na Pemba mmeisikia vizuri hivyo hakikisheni amani na utulivu vinalindwa,” amesema.
Rais Magufuli alifanya ziara ya kikazi Unguja na Pemba kwa ajili ya kutoa shukrani kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.
|
0 Comments