Afisi ya kampeni ya mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump imetoa taarifa ikisema sasa anaamini Rais Obama alizaliwa nchini Marekani.
Hilo limetokea saa chache baada ya mahojiano na Bw Trump, ambapo mgombea huyo kwa mara nyingine alisisitiza kwamba hayuko tayari kuamini kwamba Bw Obama alizaliwa Marekani. Akihojiwa na gazeti la Washington Post, Bw Trumo alikataa kusema Bw Obama alizaliwa Marekani na badala yake akasema hangejibu swali hilo.
Bw Trump huchukuliwa mwanzilishi wa kundi lijulikanalo kama "birther movement", ambalo huamini Rais Barack Obama hakuzaliwa katika jimbo la Hawaii, na kwa hivyo hakufaa kuhudumu kama rais wa Marekani.
Mwandishi wa BBC Anthony Zurcher anasema hatua hiyo itakuwa kubwa na sasa huenda ikasitisha mzozo huo.
Anasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na mshauri mkuu wa Trump Jason Miller hata hivyo si kwamba anakubali makosa.
Badala yake, anasema, Bw Miller aliweka lawama kwa Hillary Clinton na kundi lake la kampeni la mwaka 2008, ambapo Bi Clinton alikuwa anashindania tiketi ya chama cha Democratic na Bw Obama.
Hakuna ushahidi wa kumhusisha Bi Clinton na kundi la Birther.
Akijibu, Bi Clinton alisema kupitia Twitter kwamba mrithi wa Rais Obama "hawezi kuwa mtu aliyeongoza kundi la ubaguzi wa rangi la Birther".
Wanaopinga kwamba Bw Obama alizaliwa Marekani wamekuwa wakisema alizaliwa Kenya (babake Bw Obama alikuwa Mkenya).
Taarifa katika magazeti kadha ya Marekani zinaashiria uvumi huo ulienezwa mwaka 2008 na wafuasi sugu wa Bi Clinton ilipoanza kudhihirika kwamba mwanamke huyo hangeshinda uteuzi wa chama cha Democratic.
Madai hayo baadaye yalifufuliwa na wafuasi wa mgombea wa Republican John McCain alipoanza kuachwa nyuma na Bw Obama kwenye kura za maoni, tovuti ya Fact Check imeripoti.

Bw ObamaImage copyrightAP
Image captionBw Obama

Bw Trump alianza kujihusisha na suala hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2012.
Aprili 2011, alimtaka Bw Obama kuonyesha hadharani cheti chake cha kuzaliwa, wito ambao uliungwa mkono na wanasiasa wengi wa Republican akiwemo aliyekuwa gavana wa Alaska Sarah Palin.
Mwaka 2012 mgombea wa wakati huo wa Republican Mitt Romney alirejelea madai hayo kwenye mkutano wa kampeni Agosti mwaka huo.