Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema Rais John Magufuli, hana baya alilolitamka katika mikutano yake ya Unguja na Pemba, bali amezika upotoshaji wa siasa uchwara, kusafisha upepo mchafu na kufumba vinywa vya wanasiasa wakorofi na wazushi.

Pia umetoa mwito kwa Wazanzibari kwa nguvu zote kupinga siasa chafu au zenye lengo la kuwagawa, kuwatenganisha au kuwahasimisha badala yake watambue umuhimu wa kuendeleza umoja, amani na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo ofisini kwake Makao Makuu ya CCM, Dodoma, alipotakiwa kueleza maoni yake kuhusu shutuma anazotupiwa Rais Magufuli ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa kwamba alilenga kuamsha joto la mtafaruku wa kisiasa visiwani humo.
Shaka alisema hotuba ya Rais Dk Magufuli imezima siasa za uzushi na dhidi ya viongozi wanaowadanganya wafuasi wao kwamba utafanyika Uchaguzi Mkuu mwingine kabla ya mwaka 2020 na Rais Ali Mohamed Shein ataondoka madarakani ili kumpisha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wananchi wamekuwa wakipotoshwa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeshitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), The Hague, Uholanzi. Shaka alisema hotuba ya Rais ilikuwa yenye mashiko na maudhui, makatazo, maonyo, maelezo na wosia uliojiegemeza katika kudumisha amani nchini.
“Kuhubiri amani ni dhamana yake kiutawala, kuwaonya wananchi wanaokata mikarafuu, kutoboa mitumbwi, kufyeka mazao mashambani na wengine kukataa kuwauzia bidhaa wenzao halikuwa kosa na si jambo baya kama inavyoelezwa na wazushi wa kisiasa,” alisema Shaka.
Aidha, alisema ikiwa kuna mwanasiasa asiyemtii Rais aliye madarakani Zanzibar na hata kukataa hata mkono wake, hakuna sababu kwa kiongozi huyo kutaka msaada kwenye serikali asiyoitambua.
“Iweje baniani mbaya kiatu chake dawa, unajigamba humtambui Rais aliyeshinda na kuunda serikali ila unadoea fedha zinazokusanywa na serikali usioitambua ili usaidiwe na kulipwa marupurupu. UVCCM inaunga mkono SMZ kumnyima stahili zote hadi atakaipomtambua Rais,” alisema Shaka.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema wakati wa utawala wa Dk Salmin Amour Juma, Maalim Seif aliposema hamtambui kama mshindi halali hakuwa akilipwa chochote, Rais mstaafu Amani Abeid Karume hakumlipa kitu hadi alipojipeleka Ikulu Novemba 5, 2009 akatangaza kuitambua serikali yake.
Alisema matamshi ya Dk Magufuli katika hotuba zake zote, ameweka bayana kila kitu, amewakanya wanasiasa wachochezi na hatarishi kwa amani, amewaonya viongozi katika serikali zote huku akikataa uzembe, urasimu, ubadhirifu wa mali za umma na kusema wote wasiotosha, wajipime iwapo bado wanafaa au la.