Waandishi wa habari nchini Kenya wameandamana Nairobi na miji mingine kupinga kile wanachosema ni kuongezeka kwa visa vya wanahabari kutishiwa na hata kuuawa.
Maandamano yaliitishwa na Chama cha Waandishi wa habari ambacho kinasema wanahabari watano wamefariki katika hali ya kutatanisha katika kipindi cha mwaka mmoja.
Maandamano yamefanyika siku kadhaa baada ya mwandishi wa habari za kisiasa kufariki katika mazingira ya kutatanisha eneo la Kilifi, pwani ya Kenya.
Katika waraka wao walioutuma kwa bunge waandishi hao walilalamika kuhusu namna wanavyoshambaliwa na kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa wanasiasa na umma.
Wamesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wa serikali kuu, kaunti pamoja na raia wamekuwa wakijiamulia wenyewe kuchukua sheria mkononi kuidhinisha mateso na kuwashambulia waandishi wa habari kwa kuwapiga na kuwatusi kwenye mitandao ya kijamii na baadhi yao kuwatishia mauaji ikiwa hawatatoa taarifa zinazowapendelea.
Wamesisitiza kuwa wanayo haki ya kikatiba ya kutangaza taarifa.
Taarifa yao imeongeza kuwa visa hivi dhidi ya waandishi wa habari huenda ni njama za wadau wa serikali na watu binafsi za kutaka kudhibiti juhudi za waandishi wa habari wanaoripoti taarifa kuhusu , haki za jamii, wizi wa ardhi na ufisadi zififie.
Waandishi wa habari watano wameuawa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nchini Kenya.
0 Comments