Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema wanajeshi 6,000 wataondoka uraiani na kurudi kambini mwaka huu baada ya nyumba zao kukamilika.
Aidha, wizara hiyo inaweka alama katika maeneo yote ya jeshi ili kuondoa migogoro na wananchi na kuwalipa fidia wote waliovamia maeneo hayo ili waondoke.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Tunatekeleza, kinachoandaliwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na Kituo cha Televisheni cha Taifa cha TBC1.
Dk Mwinyi alisema kwa sasa wameingia mkataba na kampuni, inayojenga nyumba kwa ajili ya makazi ya wanajeshi 10,000 na utekelezaji wa nyumba 6,000 umeanza na zinakaribia kukamilika.
Alisema lengo ni kujenga nyumba hizo nchi nzima katika kila eneo lenye kambi, lakini awamu ya kwanza imechukua baadhi ya mikoa kwa kujenga nyumba 6,000 na baadhi ya mikoa itakuwa awamu ya pili nyumba 4,000.
“Kwa awamu ya kwanza nyumba hizo zitakamilika mwaka huu na awamu ya pili tunategemea kuanza mchakato na tunategemea kukamilisha mapema iwezekanavyo lakini itategemea na mazungumzo,” alisema.
Kuhusu migogoro ya wanajeshi na wananchi, alisema inatokea kutokana na awali jeshi lilikuwa likipewa maeneo bila hati, lakini baada ya ardhi kuwa na thamani kumekuwa na ongezeko la watu wanaoingia katika maeneo hayo na kuzua migogoro.
Dk Mwinyi alisema kipaumbele katika bajeti ya mwaka huu ni jeshi kupata zana na vifaa wanavyohitaji kwa majeshi yote na wameingia mikataba na zana hizo zitaanza kuingizwa nchini na kulipa kwa miaka mitano mpaka saba wakati vifaa vinavyohitajika vimeishapokelewa.