Gambia inasema itajitoa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC baada ya kuishutumu kwa kuwa aibisha Waafrika.
Taifa hilo dogo la Afrika magharibi linajiunga na Afrika kusini na Burundi katika kutangaza kujitoa katika mahakama hiyo.

Mahakama ya ICC iliundwa kusikiliza kesi mbaya zaidi duniani lakini imeshutumiwa kwa kuwalenga kwa njia zisizo za haki viongozi wa Afrika.
Waziri wa habari nchini Gambia Sheriff Bojang amesema mahakama hiyo imepuuza uhalifu wa kivita wa mataifa ya magharibi.
Amesema ICC, kwa mfano imeshindwa kumshtaki aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuhusu vita nchini Iraq.
Akizungumza kwenye televisheni, amesema ICC, ni mahakama ya 'watu weupe wenye nywele za singa ya kuwashtaki na kuwa aibisha watu wasio weupe, zaidi Waafrika'.
Mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama hiyo, Fatou Bensouda, alikuwa waziri wa sheria Gambia.
Rais Yahya Jammeh ameitawala Gambia tangu alipoingia madarakani kupitia mapinduzi mnamo 1994.
Uchaguzi unatarajiwa Desemba, lakini kiongozi wa upinzani Ousainou Darboe na wengine 18 wamefungwa kwa miaka 3 maema mwaka huu kufuatia maandamano ynayaosemekana kuwa ya haramu.
Nchi hiyo imekuwa ikijaribu kuushtaki Umoja wa Ulaya katika mahakama ya ICC kufuatia vifo vya maelfu ya wahamiaji wa Afrika wanaojaribu kuingia katika bara hilo kwa boti.
Mahakama ya ICC na haki ya kimataifa:
  • Iliidhinishwa mnamo 2002
  • Sheria ya Roma iliotumika kuiunda iliidhinihswa na mataifa 123, isipokuwa Marekani
  • Inanuia kuwashtaki na kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya wanaohusika kwa uhalifu mbaya - mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binaadamu na uhalifu wa kivita.
  • katika historia ya miaka 14 ya mahakama hiyo, ni kesi dhidi ya Waafrika pekee zilizowasilishwa.
Afrika kusini wiki iliyopita imesema imeanza rasmi mpango wa kujitoa katika mahakama hiyo kwasababu imekataa kuidhinisha waranti ya kukamatwa, itakayosababisha 'mabadiliko ya utawala'.
Mwaka jana mahakama ya Afrika kusini iliishutumu serikali kwa kukataa kumkamata rais wa Sudan, Omar al-Bashir, anayesakwa na mahakama ya ICC.
Burundi pia imesema itajitoa katika mahakama hiyo, huku mataifa mengine ya Afrika kama Kenya na Namibia yamesema yanaweza kujitoa.