Rais wa Rwanda Paul Kagame amefanya mageuzi madogo ndani ya baraza lake la mawaziri kwa kuunda wizara ndogo inayohusu maswala ya katiba na sheria nyingine.
Mageuzi makubwa yanahusu wizara ndogo mpya iliyoundwa katika wizara ya sheria ikihusu maswala ya katiba na sheria nyingine.

Wizara hiyo ndogo imepewa Bwana Evode Uwizeyimana ambaye wengi hapa Rwanda walimfahamu kama mkereketwa wa upinzani dhidi ya utawala wa RPF kabla ya kurejea nchini miaka 2 iliyopita akitoka uhamishoni nchini Canada.
Mara tu baada ya kurejea nchini Bwana Uwizeyimana alijumuishwa katika tume ya Rwanda iliyofanya mabadiliko ya katiba ambapo rais Kagame aliongezewa muda wa kukaa madarakani.
Mageuzi mengine yaliyofanyika siyo makubwa.
Rais Kagame amembadilishia wizara Dr Diane Gashumba aliyekuwa waziri wa familia na usawa wa jinsia na kumweka katika wizara ya Afya,wadhifa uliokuwa wazi tangu kufutwa kazi kwa Dr Agnès Binagwaho miezi mitatu iliyopita.
Aidha wizara ya maswala ya nchi za Afrika Mashariki imeunganishwa na wizara ya biashara inayoendelea kuongozwa na François Kanimba.
Aliyekuwa waziri wa maswala ya jumuiya ya Afrika Mashariki Bi Valentine Rugwabiza ameteuliwa kuwa balozi wa Rwanda katika Umoja wa mataifa.