Rais wa Tanzania John Magufuli anatarajiwa kuanza ziara yake ya kikazi katika nchi jirani ya Kenya leo.
Kwenye ziara hiyo ya siku mbili, Rais Magufuli anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake na pia kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.
Barabara hiyo, ambayo inaunganisha maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini, ni moja kati ya miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambayo imekuwa ikitekelezwa na serikali ya Kenya kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo kuu.
Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya saa nne asubuhi na baadaye kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.
"Katika ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi," taarifa kutoka ikulu ya Tanzania imesema.
Ziara hiyo ya Rais Magufuli inajiri wakati ambao anakaribia kumaliza mwaka mmoja madarakani.
Katika kipindi hicho, hajakuwa akizuru sana mataifa ya nje na uhusiano kati ya serikali yake na serikali ya Rais Kenyatta umeonekana kuwa 'baridi kiasi'.
Tangu aingie mamlakani mwezi Novemba mwaka jana, amezuru tu Rwanda na Uganda.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais, Dkt Magufuli alikuwa amehudumu serikalini kama waziri wa ujenzi.
Taarifa kutoka ikulu ya Tanzania inasema ziara yake imetokana na mwaliko wa Rais Kenyatta.
Kando na kutaka kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, wachanganuzi wanasema huenda Rais Kenyatta akaitumia kumpendekeza waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bi Amina Mohammed ambaye anawania wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika (AU).
Rais Uhuru Kenyatta atamkaribisha mgeni wake jijini Nairobi, baada ya Kenyatta kukamilisha ziara ya siku mbili huko Khartoum, alipokutana na Rais wa Sudan Omar Al- Bashir.
|
0 Comments