Baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Mawasiliano Serikalini wametoa maoni juu ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ili kuuboresha na kuhakikisha unaleta manufaa kwa waandishi wa habari, vyombo vya habari pamoja na wananchi wa kawaida.

Maoni hayo yametolewa na wakuu hao wakati wakihojiwa na mwandishi wa habari hii katika nyakati tofauti ambapo wengi wameonekana kutoa mawazo chanya yenye kuboresha muswada

huo.
Akiongea na mwandishi wa habari hii, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Zawadi Msalla amesema kuwa sheria hiyo inatoa mwanya mkubwa kwa kada hiyo kuwa taaluma inayoheshimika kama zingine kwa sababu baada ya Muswada huo kuwa sheria, kada hiyo itakuwa na chombo kitakachowasimamia wanahabari.

“Uanzishwaji wa Baraza huru la Habari ambalo ni moja ya kitu kilichoainishwa na Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 iliyoitaka Serikali kuanzisha chombo huru kitakachosimamia masuala ya habari hivyo, Muswada huu utakapokuwa Sheria utakuwa umetekeleza agizo la Serikali la kuanzisha chombo huru kitakachosimamia masuala hayo”, alisema Msalla.
Ameongeza kuwa sheria hii italeta uhuru wa vyombo vya habari kwani kwa sasa mmiliki asiporidhishwa na maamuzi ya kutopewa leseni anakata rufaa inayoishia kwa waziri mwenye dhamana lakini baadae mmiliki wa chombo cha habari asiporidhishwa na maamuzi ya Mhe.waziri ana uwezo wa kwenda mahakamani.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Mkoa wa Morogoro, Andrew Chimeselaamekubaliana na uamuzi wa kuundwa kwa Bodi ya Ithibati kwa sababu bodi hiyo itakua katikati kuangalia maslahi ya wana tasnia pamoja na kudhibiti nidhamu na maadili yanayokwenda sambamba na tasnia hiyo ili kusiwepo na dharau kwa tasnia hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Englibert Kayombo ameunga mkono uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati kwa sababu itasaidia kutambua wanahabari wenye taaluma halisi katika tasnia ya habari.

“Binafsi naunga mkono jitihada zinazofanywa na wizara kurasimisha tasnia hii ya habari ili iwe na hadhi sawa na tasnia zingine hivyo ni vyema kusimamia kazi za waandishi wa habari na kuwaongoza wanahabari katika kutoa habari zenye mtazamo chanya utakaojenga taifa letu”, alisema Kayombo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Luhende Singu amesema kuwa sheria hiyo itavifanya vyombo vya habari kuajiri watu wenye taaluma ya habari tofauti na ilivyo sasa pia wananchi watarajie kupata habari za ukweli na uhakika.