Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe Gedfrey Ngupula

Na Mathias Canal, Tabora




Tatizo la Mimba za utotoni na kuozesha wanafunzi katika umri mdogo
limetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa katika jamii kwani watoto wa kike
wananyimwa haki ya kupata elimu ili kujikwamua na fikra mpya katika
uchumi na namna ya kuwa na familia bora na endelevu katika kukabiliana
na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.




Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe Gedfrey Ngupula Ameyabainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com
kuhusu mikakati ya kukabiliana na mimba za utotoni pamoja na wazazi
kuwaachisha masomo watoto wao wa kike ili kuwaozesha kwa fikra potofu
za kupata mali zikiwemo Ng'ombe na fedha.



Dc Ngulupa amesema kuwa
jambo hilo limepigwa marufuku na serikali lakini bado linafanyika kimya
kimya katika maeneo mbalimbali nchini hivyo endapo atabaini wazazi
wanaofanya hivyo kuanzia sasa watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa
sheria za Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania.



Amewataka wananchi
kuachana na dhana hiyo potofu ya kujipatia mali kupitia watoto wao wa
kike badala yake wahakikishe wanafanya kazi kwa bidii ikiwemo kuwekeza
zaidi katika elimu, kilimo na ufugaji kwani ndio njia nyepesi katika
mafanikio kuliko kuwa na mtazamo hasi.



Akizungumzia changamoto
wanazokabiliana nazo walimu katika utendaji wao ikiwa ni pamoja na uduni
wa mishahara, Kitolipwa stahiki zao baada ya kupandishwa madaraja Dc
Ngupula alisema kuwa serikali kuu kupitia Mhe Rais Dkt John Magufuli
aliahidi neema kwa watumishi wote ikiwemo sekta ya afya na elimu hivyo
amewataka walimu kuwa wavumilivu katika kipindi hiki Rais anapopitia
ripoti ya watumishi hewa aliyokabidhiwa hivi karibuni ili kujiridhisha
na kuruhusu kuajiriwa kwa watumishi wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kulipa madai ya walimu ambayo yana haki kimsingi na yamekuwa ya muda
mrefu.



Hata hivyo Dc Ngupula amesema kuwa walimu wakuu wanapaswa
kuendelea kutoa taarifa za ukweli kuhusiana na upungufu wa madawati ili
kukabiliana na kadhia hiyo ambayo imekuwa ni tatizo kubwa katika shule
mbalimbali nchini.



Alisema kuwa endapo uchunguzi anaoendelea
kuufanya utabaini kuwa kuna upungufu wa madawati ilihali tayari awali
walishatoa taarifa kuwa hakuna kadhia hiyo watachukuliwa hatua haraka
iwezekanavyo ili kutoa fundishi kwa watumishi wengine wa Halmashauri ya
Wilaya ya Nzega wanaishi kwa mazoea pasina utendaji yakinifu.



Dc
Ngupula amesema kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa katika utoaji wa
takwimu za wanafunzi hewa kwani taarifa za awali zilieleza kuwa kuna
wanafunzi hewa Wilayani Nzega zaidi ya 4000 lakini amesema kuna
uwezekana wa kuwapo na wanafunzi wengine wengi hivyo endapo kama jambo
hilo litabainika wale wote walioshiriki katika udanganyifu huo
watachukuliwa hatua za haraka kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kazi.




Ili kuelekea kwenye uchumi wa Taifa la kati kuna kila sababu ya kuwa na
Taifa imara lenye wasomi wa kutosha lisiwe Taifa la watu wajinga hivyo
ni lazima kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu kwani ndio njia
pekee ya kujikwamua na umasikini uliokithiri nchini Tanzanaia.