Mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton ameelezea masikitiko yake alipojitokeza hadharani mara ya kwanza tangu ashindwe kwenye uchaguzi wa rais nchini Marekani na Donald Trump wa chama cha Republican.
Bi Clinton, akihutubu mjini Washington DC amesema alikuwa hataki kutoka nyumbani tena.

Ameambia shirika la kuwasaidia watoto wasiojiweza kwamba uchaguzi huo umewafanya Wamarekani wengi kutafakari.
Bi Clinton aliongoza kwa wingi wa kura za kawaida lakini akashindwa kinyang'anyiro cha urais kupitia kura za wajumbe, ambazo ndizo huamua mshidni wa urais.
"Sasa, nitakiri kwamba kuja kwangu hapa halikuwa jambo rahisi," alisema alipokuwa akitunukiwa heshima na wakfu wa Children's Defense Fund.
"Kuna nyakati kadha wiki hiyo moja iliyopita ambapo nilitaka kujikunyata tu nikiwa na kitabu kizuri na nisiwahi kutoka nje ya nyumba tena."