WAKATI leo dunia ikiadhimisha Siku ya Kisukari, serikali imesema kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na ugonjwa huo, lakini ikisisitiza mikakati imewekwa kupambana na magonjwa hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linaloshauri mataifa kuchukua hatua dhidi ya kisukari, watu milioni 422 wana ugonjwa wa kisukari kwa sasa na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka mara mbili zaidi ndani ya miaka 20 ijayo.

Aidha, imefahamika kwamba watu zaidi ya milioni mbili wanakatwa miguu kutokana na maradhi hayo ya kisukari.
Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ongezeko hilo linatokana na aina za maisha za watu kwa sasa.
“Kasi ya magonjwa haya inaongezeka kwa kiwango kikubwa sana ingawa sina takwimu hapa kwa sasa kwa sababu niko mbali, lakini ongezeko ni kubwa, na hii inatokana na aina ya maisha waliyonayo watu kwa sasa,” amesema Ummy.
Aliongeza kuwa sababu kubwa ya magonjwa hayo ni ulaji wa watu wa vyakula visivyokuwa bora na hasa vile vya kusindikwa, kutokufanya mazoezi na pia kula ovyo.
Alisema serikali kwa sasa imejiwekea mikakati ili kupambana na magonjwa hayo yasiyoambukiza ambayo ni pamoja na shinikizo la damu, sukari, saratani na moyo.
“Tulikuwa tunapambana na magonjwa yanayoambukiza kama kipindupindu, kifua kikuu na mengineyo, lakini sasa na huku kwenye magonjwa yasiyoambukiza tunaona nako kasi ni kubwa," alisema.
Aidha, alisema Oktoba mwaka huu, serikali ilianzisha mkakati wa kitaifa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza baada ya kubaini ongezeko kubwa la magonjwa hayo. Alisema kabla ya kumalizika kwa mwaka huu, zitazinduliwa kampeni za mkakati huo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
“Kikubwa tutakachofanya ni kutoa elimu ya magonjwa haya, kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi, ulaji sahihi wa vyakula na aina ya vyakula ili kupunguza tatizo,” aliongeza Ummy. Alisema baada ya uzinduzi yatatolewa maelekezo katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi za vijiji nini wanatakiwa kufanya.
“Kuna watu ambao tutawaingiza katika kampeni hii ambao ni 'community workers' kila kijiji wako wawili, mbali na majukumu yao mengine watafanya pia kazi ya kutoa elimu hii kwa wananchi, pia tutatumia vyombo vya habari,” alifafanua zaidi.
Katibu wa Klabu ya Mazoezi Tabata Mawenzi, Said Mgombeni alithibitisha kuwa ufanyaji wa mazoezi humfanya mtu kuwa mbali na maradhi mbalimbali na hasa yale yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo na pia kisukari.
“Hapa kwetu tunafanya mazoezi kila siku asubuhi tunakimbia kabla ya kila mmoja hajaingia katika shughuli zake za utafutaji wa maisha, afya zetu zinakuwa imara sana tunaamini kwa kufanya mazoezi mtu anakuwa mbali na magonjwa hayo,” alisema Mgombeni.
Alisema watu wanaweza kujiunga pia na vilabu au vikundi vya mazoezi ambavyo vimeundwa maeneo mengi ya mijini ili kuweza kuungana nao kufanya mazoezi bila kupata gharama ya kwenda kwenye mazoezi ya kulipia na ambapo wanapata pia muda wa kushauriana ulaji sahihi.
Mgombeni aliwashauri watu mbalimbali kujitahidi pamoja na mambo mengine ya utafutaji wa maisha, lakini pia kupata muda angalau mara mbili kwa wiki kufanya mazoezi.
Naye Dk Patrick Mirumbe alisema watu wengi na hasa wa mijini wanakula na kunywa vinywaji vya viwandani kama vile soda na juisi pamoja na vyakula ambavyo ni hatari kwa maisha yao na hawafanyi mazoezi.
“Watu wanakunywa juisi, soda, vyakula vya kopo ambavyo vinasindikwa viwandani na bado anatoka nyumbani na gari binafsi, akifika ofisini anapanda ghorofani kwa lifti na akirudi ni hivyo hivyo na akifika nyumbani anakaa kwenye televisheni, anakula na kulala, hii ni hatari kwa afya zao,” alisema Dk Mirumbe.
Amewaasa watu mbali na kufanya mazoezi kujitahidi kula vyakula vya asili pamoja na juisi za kutengeneza za matunda. Ameshauri pia kuchunguza afya kila baada ya miezi mitatu.