RAIS Edgar Lungu wa Zambia na Rais John Magufuli wameahidi kuifumua Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kutokana na kushindwa kujiendesha kibiashara.
Viongozi hao wawili walisema katika mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam jana kwamba, suala la Tazara walilijadili kwa kina na kubaini kuwa tatizo ambalo limechangia kufifisha uwezo wa shirika hilo ni menejimenti, hivyo wameahidi kufanya mabadiliko makubwa katika eneo hilo.

Katika mabadiliko hayo, viongozi hao wamekubaliana kubadilisha kwanza sheria zinazoendesha shirika hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1976 ili ziruhusu ajira ya mkurugenzi mkuu na wasaidizi wake watoke nchi yoyote duniani kutokana na uwezo wao wa kazi. Sheria ya sasa ya Tazara inasisitiza kuwa mkurugenzi mkuu lazima aajiriwe kutoka Zambia na msaidizi wake lazima awe Mtanzania.
Kwa mujibu wa viongozi hao wawili, katika mazungumzo yao wamekubaliana kwamba wanasheria wakuu wa nchi hizo wakutane waone namna ya kubadilisha sheria hiyo.
“Tatizo la Tazara sio mtaji, maana walishakuwa na mtaji mwaka 1976 wakati shirika linaanzishwa, sisi tumebaini tatizo la shirika hilo ni menejimenti, hivyo tumekubaliana na mwenzangu kuwa lazima tubadilishe sheria kwanza ili ajira ya mkurugenzi iruhusu hata mtu kutoka Uganda, Uingereza au Rwanda,” alisema Rais John Magufuli.
Usafirishaji wa shehena unaofanywa na Tazara umeshuka kutoka kusafirisha tani milioni 5 kwa mwaka hadi kufikia tani 128,000. Kwa upande wake, Rais Lungu alisema “Lengo la nchi hizi mbili ni kuona Tazara inatengeneza faida na isaidie kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili ndio maana tumedhamiria kwamba kwa kuwa tatizo ni menejimenti lazima tupate mtu sahihi wa kuendesha shirika hilo.”
Aliongeza kuwa iwapo Tazara itafanya vizuri kwenye usafirishaji wa shehena, ni wazi kuwa matumizi ya barabara yatapungua na na pia akasisitiza kuwa nchi zote mbili zingependa kuona reli hiyo ambayo ilijengwa na China inafanya vizuri zaidi kuliko ilivyo sasa.
Eneo lingine ambalo walizungumzia viongozi hao ni suala la Bandari ya Dar es Salaam ambayo Rais Magufuli alisema Zambia ndio nchi inayoongoza kwa sasa kupitisha mizigo katika bandari hiyo na hivyo wamekubaliana kupunguza vituo vya ukaguzi na kubaki vinne.
“Pamoja na kwamba Tazara haifanyi vizuri, lakini Zambia imeendelea kutumia barabara kusafirisha mizigo kupitia bandari yetu, hawa ni rafiki wa kweli wa uchumi wa Tanzania, ni lazima tusaidie kupunguza muda wa magari kufika Zambia,” alisema Dk Magufuli.
Kuhusu Bomba la Mafuta la Tazama, viongozi hao pia walikubaliana kuhakikisha kuwa uwezo wa bomba hilo ni kusafirisha tani milioni 1.1 kwa mwaka, lakini kwa sasa linasafirisha tani 600,000 jambo ambalo alisema wamekubaliana kulifanyia kazi kubaini kwa nini kunazorota kwa namna hiyo.
Rais Magufuli pia alisema wamekubaliana gesi ya barafu ambayo imegundulika hivi karibuni ikianza kuchimbwa wajenge bomba la kuwauzia gesi hiyo inayotumika kuendesha mashine ya MRI katika hospitali.
Wakati huo huo, Rais Lungu alipoulizwa amejifunza nini katika uongozi wa Rais Magufuli, alisema ameona kwamba ni kiongozi ambaye amedhamiria kuwatoa watu wake kwenye umasikini na kuwapeleka kwenye maisha mazuri.
“Nimejifunza mengi lakini anaitwa buldoza kwa kuwa mwelekeo wake ni sahihi juu ya watu anaowatumikia na wananchi wake wanamkubali, sijui kama na mimi nakubalika kwa Wazambia kama alivyo yeye,” alisema Lungu.
Magufuli awa Lungu na Lungu awa Pombe Viongozi hao walisema kwamba walishabadilishana majina mara walipokutana huko Uganda. Rais Magufuli alisema kwamba kwa kuwa Rais Lungu anatumia kilevi alichukua jina la Pombe na yeye Magufuli kwa kuwa anaongoza kwa kutumia rungu, alichukua jina la Lungu.
“Tulipokutana pale Kampala, Uganda ndipo nilipomwona kuwa huyu ni rafiki yangu na tangu siku hiyo tukabadilishana majina,” alisema Rais Magufuli.