RAIS John Magufuli ametua Kenya na kumweleza mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufanya kazi kwa bidii ili nchi isonge mbele huku akisisitiza ‘Hapa Kazi Tu’ katika ulipaji kodi na kukabiliana na ufisadi.

Aidha, alisema Kenya ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ikilinganishwa na nchi nyingine za Bara la Afrika. Rais Magufuli aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya ambako ameanza ziara ya kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Rais Kenyatta.
“Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii ili nchi iende mbele. Tunasisitiza Watanzania walipe kodi na tunakabiliana na ufisadi,” alisema Rais Magufuli na kuitaka Tume ya Pamoja ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kukutana haraka ili kukamilisha taratibu za ushirikiano kwa sababu imechukua miaka minne sasa.
“Kule nchini nina msemo wangu kwamba ‘Hapa Kazi Tu’, hivyo lazima tufanye hili kwa haraka ili tusonge mbele kwa sababu tumekuwa tukizungumza kwa miaka minne sasa,” alisema Rais Magufuli mbele ya wenyeji wake, Rais Kenyatta na maofisa wa nchi hizo mbili.
Akizungumzia uwekezaji, Rais Magufuli ambaye kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, alipokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, alisema takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake nchini Tanzania, ambapo zimewekeza Dola za Marekani bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.
Pia, Rais Magufuli amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Sh za Kitanzania bilioni 652.9 hadi Sh trilioni 2.044.
"Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndio nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika.
"Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka,” alisema Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Dk Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya, ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na aliwakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya kuwekeza nchini.
"Kabla ya kuja hapa nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo,” alisisitiza Dk Magufuli.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na alimhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.
"Kwetu sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu,” alisema Uhuru.
Rais Uhuru alisema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu, ikiwemo kubadilishana uongozi wa serikali kwa njia ya amani na aliongeza kuwa katika mazungumzo yao, wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki, zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.
Aidha, alisema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano, ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili itayaainisha.
Jana jioni, Rais Magufuli alitarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa katika Ikulu ya Nairobi, aliyoandaliwa na mwenyeji wake na leo anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen jijini Nairobi, na kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo jijini humo. Hii ni ziara ya tatu nje ya nchi kwa Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwaka mmoja sasa. Ziara nyingine alikwenda Rwanda na nyingine Uganda.