Mmarekani Ruggy Timothy ndiye aliyeshinda raundi ya kwanza ya ufunguzi wa mashindano ya mbio za kimataifa za baiskeli maarufu Tour of Rwanda yaliyoanza mjini Kigali.
Timothy kutoka timu ya Lowestrates ya nchini Canada, ameshinda raundi hii ya kilomita 3,3 akitimka kwa dakika 4 nukta 00.

Amewashinda kwa nukta chache Aman Gebreig Zabhier kutoka Eritrea aliyeshika nafasi ta pili na Areruya Joseph wa Rwanda aliyechukua nafasi ya tatu.
Baada ya ushindi huo Ruggy ametangaza kufurahia ushindi huo:
"Raundi hii inayofahamika kitaalamu kama Prologue ni kama kionjo cha mashindano haya,kazi kubwa itaanza kesho,lakini tuna timu kabambe tumekuja kushindana kikweli ,naweza kuchukua jezi ya manjano au ikachukuliwa na mwingine lakini tuko tayari kuchuana katika milima hii ya Rwanda"
Mchuano mkali unatarajiwa kuwa baina ya timu hiyo ya Wamarekani na magwiji wa mbio za baiskeli kutoka bara la Afrika akiwemo OKUBAMARIAM TESFOM kutoka Eritrea ambaye ndiye bingwa wa Afrika.
Kuna pia bingwa mtetezi wa mshindano hayo Mnyarwanda Jean Bosco Nsengimana,huyu kwa sasa anaichezea timu ya Bike Aid ya Ujerumani,bila kumsahau bingwa wa mwaka 2014 Valensi Ndayisenga ambaye naye alisajiliwa na timu ya Dimension Data ya Afrika kusini lakini inachezea barani Ulaya.
Kesho mashindano yataanza kuelekea mikoani huku washindani 75 watatoka Kigali hadi mji wa Ngoma mashariki mwa nchi umbali wa km 100.
Kenya ndiyo nchi pekee ya Afrika mashariki inayoshiriki mashindano hayo ikiwakilishwa na timu ya Kenyan Riders Downunde.
Shindano la Tour of Rwanda ndilo la pili kwa ukubwa linalotambuliwa na chama cha mbio za baiskeli barani Afrika nyuma ya shindano la kimataifa la Amisa Bongo la nchini Gabon.