WATU sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Yusuf (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kwa jina la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, huku baadhi wakiwa hawajavaa viatu, wakitembea kwa kuchechemea.

Baada ya kusomewa mashtaka, upande wa Jamhuri ulidai unatarajia kuwapeleka washtakiwa hao katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama “Mahakama ya Mafisadi” kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Washtakiwa hao watapelekwa katika mahakama hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuandaa maelezo ya mashahidi pamoja na vielelezo ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Yusuf pamoja na wenzake Charles Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46) walisomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Thomas Simba.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Paul Kadushi alidai katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aliendelea kudai kuwa katika shtaka la pili kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vyenye thamani ya dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.
Katika mashtaka mengine, inadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, washtakiwa wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.7.
Aidha, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori. Hakimu Simba alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu mashtaka yao kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo aliiahirisha hadi Desemba mosi mwaka huu.
Kabla ya kutoka kwenye chumba cha mahakama, washtakiwa walimuomba hakimu awape muda waeleze jinsi walivyokamatwa kwa kuwa walipigwa sana. Mpemba alidai siku aliyokamatwa, alipigwa sana hadi sasa hawezi kusikia vizuri na viungo vyake vya mwili havina nguvu hivyo aliomba PF3 ili akatibiwe.
Mrutu alidai kuwa alipigwa hadi wakamng’oa kidole kimoja cha mkononi na washtakiwa wengine walidai walipigwa mpaka sasa wanashindwa kutembea vizuri hivyo waliomba wapewe msaada wa kutibiwa.
Hakimu Simba alisema hawezi kutoa amri ya kutolewa kwa PF3 kwa sababu Magereza wana zahanati zao na kuna taratibu wanazifuata hivyo wasiwe na wasiwasi na kama watashindwa kuwatibia, watatafuta utaratibu mwingine wa kuwapeleka katika hospitali za nje ya Magereza.
Baadhi ya washtakiwa, waliingia mahakamani hapo wakiwa wanachechemea huku wakificha sura zao kukwepa kupigwa picha. Washtakiwa wawili hawakuwa na viatu.