Rais John Magufuli akifurahia jambo na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi baada ya kumaliza mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu)
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema Rais John Magufuli ameleta tsunami kwa wabadhirifu wa fedha za umma kupitia falsafa yake ya kutumbua majipu.
Aliyasema hayo jana wakati alipokutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo, Ikulu Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kiongozi huyo aingie madarakani mwaka mmoja sasa.

Kupitia falsafa yake ya kutumbua majipu, Dk Magufuli amechukua hatua za kuwasimamisha na kuwafuta kazi baadhi ya watumishi wa umma wakiwemo wakurugenzi wa taasisi nyeti.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilifafanua kuwa baada ya mazungumzo hayo, Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo ni kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani na pia kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Mwinyi aliyataja baadhi ya maeneo ambayo Rais Magufuli ameyafanya kwa mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa na akabainisha kuwa hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.
"Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya Mwalimu Nyerere, aliipondaponda kabisa lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta tsunami, nafurahi sana,” alisema Mzee Mwinyi.
Eneo jingine ni kuimarisha utendaji kazi serikalini ambao Mwinyi alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Rais Magufuli zimeongeza kasi zaidi na ametoa mwito kwa viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.
“Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumuombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo watu wanapotosha, tuseme sio hivyo, ilivyo ni kadhaa kadhaa kadhaa, tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri nzuri ya ajabu,” alisisitiza Rais mstaafu Mwinyi.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amewafuta kazi na wengine kusimamishwa watumishi takribani 160 wakiwemo wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma, wakurugenzi wa taasisi za umma, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala wa mikoa na watumishi wengine wa serikali wakiwemo wa taasisi nyeti kama Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Mara tu baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah kwa kile alichoeleza kuwa ni kutokana na kutoridhika na utendaji wa taasisi hiyo katika mapambano ya rushwa.
Wamo watumishi wengi ambao wameondolewa na Rais Magufuli madarakani na wengine tayari wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ubadhirifu na wengine bado wanachunguzwa na mamlaka mbalimbali.
Kutokana na juhudi hizo, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, wananchi, viongozi wa dini na wasomi wamekuwa wanapongeza hatua hizo zinazochukuliwa na Rais za kupambana ufisadi pamoja na kuleta nidhamu katika utendaji wa serikali.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk Reginald Mengi akitoa tathmini ya uongozi wa Rais Magufuli mwaka mmoja tangu aingie madarakani, alisema "Tofauti na awamu zilizopita, ambapo watumishi walikuwa wakikiuka miiko ya utumishi wa umma, lakini hawachukuliwi hatua za dhati, awamu hii tumeshuhudia hatua zikichukuliwa mara moja chini ya kaulimbiu ya ‘utumbuaji majipu.
"Huko nyuma kulikuwa na kuundwa kwa tume kila mara eti kuchunguza waliokiuka au wanaotuhumiwa maadili, na ripoti za uchunguzi zilipokamilika, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa. Leo hii mtu akiharibu, hakuna cha kuunda tume, anatumbuliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi. “Mafanikio yote haya yamepatikana katika mwaka mmoja tu wa serikali ya awamu ya tano. Na lazima tukubali kwamba huu ni mwanzo mzuri," alisema Dk Mengi katika tathmini yake juu ya uongozi wa Rais Magufuli.
Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano Mkuu wa Chama cha ACT–Wazalendo, Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto alisema chama chake kinaunga mkono na kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Magufuli, za kusafisha serikali na kuimarisha utawala bora.
Zitto alisifu kasi ya vita dhidi ya ufisadi na rushwa, kurudisha uwajibikaji katika utumishi wa umma, licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa kwenye sekta za elimu, uchumi na utawala bora.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana katika tathmini yake juu ya uongozi wa Rais Magufuli alisema ni zawadi kutoka kwa Mungu kutokana na jinsi alivyoamua kuisafisha serikali ambayo watendaji wake walijaa uozo mkubwa.