Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, mwenye umri wa mika 92, anazungumzia kuhusu kustaafu , lakini swali ambalo bado watu wanahoji ni ikiwa kweli anamaanisha hilo.
Mwishoni mwa juma Bwana Mugabe aliuambia mkutano wa watu wapatao 400- walio piagania uhuru kwamba ikiwa atastaafu anapaswa kupewa fursa "inayofaa" kufanya hivyo.
Pia aliwakosoa baadhi ya viongozi wa chama chake cha Zanu-PF kwa kumuombea afe na kujaribu kumroga ili wachukue nafasi yake.
Malumbano ya ndani kwa ndani miongoni mwa wafuasi wa chama tawala ya kutaka kumrithi Bwana Mugabe yameongezeka huku kiongozi huyo akionekana kuendelea kudhoofika zaidi.
Lakini si mara ya kwanza Kwa Bwana Mugabe kuongelea kuhusu kuachia madaraka.
Mwaka 2006 alitangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2008.
Licha ya hayo aligombea na kushinda katika uchaguzi uliokuwa na ghasia ambao matokeo yake yalibishaniwa.
Kwa hivyo haijawa wazi ni lini , kama kweli Rais Mugabe ataondoka madarakani.
Mnamo mwishoni mwa juma kamati za kikanda za chama tawala cha, Zanu-PF zilimuidhinisha kama mgombea wake katika uchaguzi wa 2018, ambapo atakuwa na umri wa miaka 94.
Chama hicho kitaidhinisha uamuzi huo katika mkutano mkuu wa chama utakaofanyika mwezi ujao.
Kwa hiyo kwa sasa haionekani kama kweli anaangalia uwezekano wa kustaafu.

maandmanoImage copyrightAP
Image captionUtawala wa Mugabe umekuwa ukikumbwa na maandamano huku wanaharakati na raia kwa ujumla wakimtaka rais Mugabe aachie mamlaka.
Maandamano
Image captionMaandamano ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi Zimbabwe

Utawala wa rais Mugabe umekuwa ukikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa sarafu ya nchi hiyo.
Hali mbaya ya uchumi na ukosefu wa ajira vilisababisha maandamano makubwa kote nchini humo, wanaharakati na raia kwa ujumla wakimtaka rais Mugabe aachie mamlaka.
Hata hivyo Mugabe amekuwa akiyazima maandamano hayo na kuwatia nguvuni wapinzani wake anaosema kuwa wanachochewa na mataifa ya kigeni. kutokana na vikwazo kutoka mataifa ya magharibi.
Mugabe amekuwa akikosolewa kwa kukandamiza upinzani.