Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Yamungu Kayandabila
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema migogoro ya ardhi nchini bado ni changamoto, lakini katika mwaka mmoja wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano migogoro 1,378 imefika wizarani na 690 imetatuliwa kiutawala.
Aidha, katika mwaka huo tayari maandalizi ya Sera ya Makazi ambayo inapitiwa na Chuo Kikuu cha Ardhi na Marekebisho ya Sera ya Nyumba yanakamilishwa.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Yamungu Kayandabila alisema hayo wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachoandaliwa na kurushwa hewani na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kisha katika ufafanuzi kwa gazeti hili jana.
Dk Kayandabila alieleza kuwa katika miezi 12 ya utawala wa Rais John Magufuli migogoro 1,378 imefika wizarani na 690 imetatuliwa kiutawala, huku akifafanua kwamba migogoro ya ardhi hutatuliwa kiutawala na kisheria kwa kufuata mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata, wilaya, nyumba hadi katika ngazi ya Mahakama ya Rufani.
Alisema migogoro hiyo iliyotatuliwa wizarani ni mbali na iliyotatuliwa na Kamati za Ardhi Vijijini, Kata, Wilaya na mabaraza mengineyo ambayo yanafanya kazi zake kama Mahakama.
Dk Kayandabila alisema migogoro mingi ya ardhi inatokana na kutozingatiwa kwa sheria na taratibu zilizopo kwani tangu mwaka 2004, mabaraza ya ardhi 117,400 yalikaa na kufanya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya mashauri zaidi ya 103,000. Kwa wastani kwa mwaka mabaraza hayo yanatatua migogoro zaidi ya 12,000.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alifafanua kuwa mabaraza mapya 47 yameundwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Awamu ya Tano, mabaraza matatu kati ya hayo yamezinduliwa na kuanza kazi Lushoto na Kilindi mkoani Tanga na Kiteto katika mkoa wa Manyara.
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo ndiyo inayotekelezwa na serikali, imeelekeza kuundwa kwa mabaraza 100 katika kipindi cha miaka mitano, lakini kwa mwaka mmoja tayari yameundwa mabaraza 47, hali inayoashiria kuwa utekelezaji huo utavuka malengo kwa asilimia kubwa.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa migogoro ya ardhi inatokana na kuwa wakati wa Uhuru kulikuwa na watu milioni 12, lakini sasa wamefikia watu milioni 50 huku mifugo ikiwa milioni tatu kwa wakati huo, lakini sasa imefikia milioni 25.
“Watu na mifugo inaongezeka, lakini ardhi haiongezeki hivyo kuibuka matatizo ya ardhi jambo ambalo sasa tumejipanga kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa ardhi iliyopimwa kwa kuwa na kituo cha huduma kwa mteja ili kuwezesha kupata hati kwa urahisi wizarani,” alieleza Dk Kayandabila.
Akizungumzia mji mpya wa Kigamboni, alisema sasa wako katika maandalizi ya kukamilisha Mpango Kabambe wake na tayari hati 291 zimetolewa. Alisema awali upangaji wa mji huo ulisimamishwa, lakini baada ya kupatikana kwa Manispaa ya Kigamboni na kubaki na kata sita badala ya tisa, wameanza upya.
“Hakika wizara yangu bado inakabiliwa na changamoto ya watumiaji ardhi pamoja na ukosefu wa kumbukumbu mbalimbali za ardhi na sasa wametengeneza mifumo unganishi ili kukabiliana na changamoto hizo,” alieleza.
Dk Kayandabila aliwataka wananchi kuzingatia sheria kwa kuacha uvamizi katika maeneo wasiyoruhusiwa huku akiwataka watumishi kuacha kujiona ni wafalme, bali kutumikia wananchi kwa tafsiri ya utumishi wa umma iwe kwa vitendo.