Baraka Elias Mashauri, ni kijana Mtanzania mrefu wa futi 7.4, urefu wake usio wa kawaida umemfanya kushindwa kupata matibabu ya kubadilishiwa nyonga baada ya kuanguka nyumbani kwake.
Akizungumza na BBC akiwa nyumbani kwake nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Elias amesema ameshindwa kupata matibabu kwa sababu kimo chake.
Elias alipelekwa kwenye Taasisi ya tiba ya mifupa ya Muhimbili, MOI kwa ajili ya uchunguzi wa madaktari, akitokea mkoa wa Ruvuma kusini mwa Tanzania, baada ya kukosa huduma kwa kile kilichoelezwa kutokuwa na wataalam na vifaa vya kumtibu.
''Madaktari wa MOI wamesema kuwa vifaa walivyonavyo na wagonjwa waliozoea kuwahudumia ni tofauti na mimi," amesema.
"Hata vifaa vya X-Ray haviwezi kutoa picha halisi ya kuona ukubwa wa kifaa wanachopaswa kuniwekea, pia wamesema vitanda vya kulaza wagonjwa wakifanyiwa upasuaji ni vifupi kwa kuwa mgonjwa anapaswa mwili wote uenee kitandani''.
Baraka Elias
Kutokana na hali hiyo Elias sasa anasubiri majibu ya madaktari ambao wanafanya mazungumzo na wenzao wanaoshirikiana nao katika shughuli za kitabibu nje ya Tanzania, ili aweze kupata matibabu.

Kurithi

Elias amesema jamii inayomzunguka hushangaa urefu wake, lakini anasema kwake anaona kawaida tu kwa kuwa wazazi wake walimweleza kuwa urefu wake ni wa kurithi.
''Upande wa familia ya Baba na Mama babu zao wote walikuwa warefu kwa hiyo hii hali nafikiri imesababishwa na vinasaba''.
Baraka Elias
Image captionBaraka Elias akiwa amesimama na mwandishi wa BBC Lizzy Masinga