Moses Machali
ALIYEKUWA Mbunge wa Kasulu kupitia NCCR-Mageuzi, Moses Machali amehamia katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) akitokea Chama cha ACT-Wazalendo ili aunge mkono jitihada za utendaji kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Katika taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana, ambayo mwanasiasa huyo amelithibitisha gazeti hili kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kuwa ni yake, alisema ni aibu kwa mtu yeyote makini na anayehitaji mabadiliko kushindwa kuunga mkono jitihada za Dk Magufuli.

“Mimi Moses Joseph Machali niliyefanya sana siasa za upinzani hapa nchini na niliyepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala nchi hii; niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa nguvu na uwezo wangu wote nikishirikiana na wapinzani wenzangu, ninaamua kujiunga na watu wanaonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi yetu,” alisema Machali.
Alisema watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga Tanzania kwa maendeleo endelevu ni jamii ya viongozi kama Dk Magufuli, Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, mawaziri na viongozi wengine walioko chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Machali aliyeanza safari yake ya siasa tangu mwaka 2007 hadi 2010 akiwa Chadema, 2010 hadi 2015 akiwa NCCRMageuzi na 2015 hadi 2016 alipojiunga na ACT na sasa CCM, alisema mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi wake unatosha kwa mtu yeyote makini kufanya uamuzi wa kumuunga mkono.
“Mimi nimechagua kumuunga mkono Rais kwa vitendo, kwa sababu ninaposoma rekodi yangu ya enzi nikiwa mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge nilipinga mno wizi na ufisadi wa kila aina; Nilipinga Matumizi ya fedha serikalini yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa,” alisisitiza.
Alisema kutokana na jitihada zake kwa kushirikiana na wabunge wengine wa upinzani katika kupinga ufisadi, leo Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha kasi nzuri katika kuwachukulia hatua watu hao. “Hata hivyo, leo hii upinzani umepoteza mwelekeo kwa sababu unapingana na kile ilichokihubiri nchini.
Ajenda ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena, bali ya JPM na CCM yake au yao. Wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia na kuyahubiri huko nyuma. Hakika huo si uungwana, bali aina mpya ya ufisadi nchini na usaliti kwa agenda zao,” alisisitiza mwanasiasa huyo kijana aliyekuwa machachari bungeni.
Alisema taifa haliwezi kuwa na siasa za kutokukubaliana na ukweli unaoishi na kusisitiza kuwa endepo Watanzania wakiwemo wapinzani wanataka kuwa na taifa linaloendelea, waachane na watu wanaopinga kila kitu hata yale yaliyo mema na badala yake waunge mkono mambo hayo mema bila kujali yanafanywa na nani.
Alisema kwa sasa nchi inavyoonekana ni kama inasukwa upya na kuwataka Watanzania wawaunge mkono viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuijenga nchi hiyo.
“Tuachane na siasa nyepesi za kutaka kuona kwamba mazuri ni yale yanayofanywa na wapinzani huku mambo hayohayo yakifanywa na CCM yanaonekana hayafai. “Hivyo basi, leo ninatangaza rasmi kwamba ninajiunga na timu JPM kwa maslahi ya taifa kwa kuwa sioni sababu ya kupingana na yale niliyoyapigania na itakuwa ni sawa na mtu kupigana na kivuli chake mwenyewe. Kwaherini Upinzani nimeamua kuanza siasa mpya za masuala yale niliyoyaamini na ninayoyaamini. Imani ni Matendo Na Matendo ni imani. Piga vita ufisadi kwa imani na Matendo,” alisema Machali.
Naye Fadhili Abdallah kutoka Kigoma, anaripoti kuwa, CCM mkoani Kigoma inaandaa mapokezi makubwa kwa ajili ya kumpokea mwanachama wake huyo mpya.
Katibu Mwenezi wa CCM mkoani humo, Masudi Kitowe alithibitisha Machali kujiunga na CCM na kukabidhiwa kadi yake ya kujiunga na chama hicho mkoani Dodoma juzi.
Kitowe alisema baada ya taarifa hizo aliwasiliana na Machali ambaye alimthibitishia hilo na kwamba CCM Wilaya ya Kasulu Mjini inamuandalia mwanachama huyo mapokezi makubwa siku atakayorejea wilayani humo.
Alisema hawajajua ni lini Machali atarejea mkoani Kigoma na hasa nyumbani kwao wilayani Kasulu ingawa mawasiliano kuhusu kurejea kwake nyumbani yanaendelea.