Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga
TANZANIA na Zambia zinatarajia kusaini mikataba minne ikiwemo ya usafirishaji ambayo Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), itasaini mkataba utakaowezesha ndege zake kufanya safari za Lusaka, Zambia.
Pamoja na mikataba hiyo, viongozi wa nchi hizo mbili watapokea mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyofanyia kazi matatizo ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuangalia jinsi ya kutekeleza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga alisema matukio hayo yatafanyika baada ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu kuwasili nchini keshokutwa kwa mwaliko wa Rais John Magufuli.
Alisema Rais Magufuli amemwalika Rais Lungu nchini kwa ziara ya siku mbili ambapo Jumatatu atazuru vituo vya kuunganisha nchi hizo mbili ikiwemo Tazara.
Alisema katika ziara hiyo, mikataba minne itasainiwa ikiwemo ya usafirishaji, ambapo ATCL itasaini mkataba wa safari za ndege zake kwenda Lusaka ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo.
Pia, viongozi hao watagusia Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) ili kuona uwezekano wa kulitumia kusafirisha mafuta ghafi, mafuta safi na gesi.
“Viongozi wetu na wataalamu wetu wataangalia pia uwezekano kama bomba la mafuta la Tazama litaweza kufanya kazi zaidi ya moja yaani litumike kusafirisha mafuta ghafi, safi na gesi na kama haiwezekani wataangalia kama upo uwezekano wa kulipanua au kujenga jingine pembeni,” alisema Balozi Mahiga.
Aidha, alisema katika mazungumzo baina ya viongozi hao, watazungumzia jinsi ya kutafuta suluhu ya matatizo ya Tazara, ambapo awali kikao cha wataalamu kikiwajumuisha wataalamu wa Zambia na Tanzania, walikaa kuangalia jinsi ya kuboresha na kutatua matatizo ya mamlaka hiyo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Grace Mwijuma, alisema ziara hiyo itafungua ukurasa mwingine wa uhusiano baina ya nchi hizo na kwamba zaidi ni kwa Bandari ya Dar es Salaam kuangalia jinsi ya kuboresha huduma ili wafanyabiashara wa nchi hiyo warudi kuitumia.