RAIS John Magufuli amevitaka vyuo vya elimu ya juu nchini kuhakikisha vinatoa elimu bora kwa kuwa suala la ubora wa elimu nchini halina siasa wala mjadala na hakuna njia ya mkato kuipata.
Pamoja na hayo, alisema wakati serikali yake ilipotangaza elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, kuliibuka changamoto kadhaa kutokana na ongezeko la wanafunzi, ikiwemo kubaini wanafunzi hewa 65,000.
Dk Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika Kampasi Kuu iliyopo Bungo, wilayani Kibaha, Pwani.

Alisema kutokana na kutaka kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walipohakikiwa walikutwa wenye sifa za kuwa chuoni hapo ni wanafunzi 322 kati ya 7,500.
“Tumeamua kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora. Wanafunzi hao wa Udom tuliwahamishia vyuo vingine kulingana na sifa zao, hivyo tungependa kila mtu asome kwa sifa aliyonayo na si vinginevyo. Tungependa sifa ya elimu yetu iwe juu. Ni bora kuwa na wanafunzi wachache kuliko kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wasio na sifa,” alisema.
Kuhusu elimu bure, alisema serikali ilipoamua kufanya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari kulijitokeza changamoto nyingi ambapo wanafunzi wa shule za msingi waliongezeka kutoka milioni moja hadi milioni mbili ikiwa ni ongezeko la idadi ya wanafunzi kwa asilimia 84 kwa shule za msingi na asilimia 26 kwa sekondari kidato cha kwanza.
“Ziliibuka changamoto za madarasa na madawati, madawati tumepambana na sasa imefikia asilimia 98 ambapo mikoa michache inamalizia. Pia kuliongezeka wanafunzi hewa 65,000 kwa shule za msingi na sekondari ambao walikuwa wakilipwa malipo hewa kwa kuongezwa majina ya uongo. “Changamoto zilizidi kuongezeka kwani bajeti ya mikopo iliongezeka kutoka Sh bilioni 340 na kufikia Sh bilioni 473 kutokana na ongezeko la wanachuo kutoka 98,000 hadi kufikia 124,389,” alisema Magufuli.
Dk Magufuli alisema wanafunzi waliokuwa wanapewa mikopo hewa kwenye vyuo hadi sasa imefikia Sh bilioni 3.5 kiasi kilichowahi kusemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako Agosti 17, mwaka huu, alipotoa taarifa kuhusu uhakiki wa vyuo vikuu nchini kuwa umebaini wanafunzi hewa walipewa mikopo ya kiasi hicho cha fedha na kutoa siku saba, vyuo husika virejeshe fedha hizo.
Aidha, alisema OUT nayo ina sifa kama vyuo vikuu vingine ambavyo vinatoa elimu ya moja kwa moja hivyo nayo inatakiwa kudahili wanafunzi wenye sifa kwani wanapokwenda kwenye ajira haiangaliwi amesoma chuo gani.
Awali, Waziri Profesa Ndalichako alisema kuwa chuo hicho kinasaidia kuongeza wasomi nchini ambapo kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wanaojiunga na chuo hicho ambapo asilimia 90 wanaosoma ni watumishi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda alisema kuwa wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu bora na wamewapatia elimu baadhi ya watu wengi ambao kwa sasa ni viongozi wa ngazi za juu.
Profesa Bisanda alisema elimu hiyo wanayoitoa kwa masafa kwa gharama nafuu kwa sasa wamejitanua kwenye baadhi ya nchi kama Rwanda, Kenya na nchi nyingine.