MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2016 unatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, ukigusa sheria tisa ikiwemo ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo sasa mnufaika wa mkopo aliyejiajiri atalipa kiasi kisichopungua Sh 120,000 au asilimia 15 ya kipato chake, huku taasisi za umma, bodi, wakala na tume zimebanwa zisirekebishe au kuwianisha mishahara, posho na marupurupu kwa watumishi.

Kwa mujibu wa muswada huo, kwenye Sheria ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, waajiri wanaoshindwa kuwasilisha marejesho ya mwezi baada ya makato wataadhibiwa, ambapo mwajiri atawajibika kuitaarifu Bodi ya Mikopo kuhusu ajira ya mtu yeyote ambaye ana shahada au stashahada na kukata makato ya mwezi kutoka kwenye mshahara wa mnufaika wa mkopo.
Kifungu hicho kinapendekeza kufanya marejesho ya mkopo kuwa ya kisheria na kupewa nafasi ya awali katika orodha ya makato na kinapendekeza kupunguzwa idadi ya wajumbe wa Bodi ya Mikopo na kufikia saba kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji.
Mishahara, posho za watumishi
Kwenye marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Kifungu cha 8 kinapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Katibu Mkuu (Utumishi) kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma.
Inapendekezwa kumuondolea Katibu mamlaka ya kuteua watumishi wa umma wanaounda baraza la majadiliano ya pamoja ya watumishi wa umma na sasa waziri atateua katibu kutoka wizara yenye dhamana na kada husika ya watumishi.
Pia inapendekezwa kufuta kifungu cha 11 ili kuondoa masharti yanayokataza Baraza la majadiliano ya pamoja ya watumishi na baraza la pamoja la watumishi wa umma kutoa mapendekezo kuhusu ujira.
Faini papo hapo ukikiri kosa Kwa upande wa marekebisho ya Sheria ya Leseni na Usafirishaji, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kutaongezwa kifungu ili kuweka masharti yanayoruhusu ulipwaji wa faini pale mkosaji anapokiri kosa, badala ya kila kosa kufuata taratibu za kimahakama.
Muswada huo una marekebisho kwenye Sheria ya Mazingira ambako kutawekwa mwongozo wa namna ya kupima urefu wa mita 60 kwenye kingo za bahari, ziwa, mto au bwawa la maji kinachozuiliwa kufanyia shughuli zozote za binadamu. Upimaji utapimwa kuanzia kwenye kingo za maeneo hayo.
Sheria nyingine zitakazofanyiwa marekebisho kwenye Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 ni ya Usafiri wa Anga, Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Vipimo.
Spika Job Ndugai wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Tano wa Bunge wiki iliyopita, alieleza kuwa kwa wiki hii Bunge litapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG) ya mwaka 2014/2015 kisha kujadili na kuishauri serikali kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na Afrika Mashariki (EPA-EU) na kisha taarifa ya kamati ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo.