Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuk
WATUMISHI hewa 19,629 wamebainika kuwapo nchini tangu uhakiki ufanyike; na kama wangelipwa, serikali ingepoteza Sh bilioni 19.7 kwa mwezi.
Aidha, kutokana na hali hiyo, serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi 1,663 kutoka katika taasisi zake kwa watumishi waliohusika na kuwepo kwa watumishi hewa na kati ya hizo, watumishi 638 wamefunguliwa mashtaka polisi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema bungeni mjini hapa jana kuwa serikali ingepata hasara hiyo, endapo watumishi hao hewa wangelipwa kwa mwezi.
Akitoa mfano wa halmashauri mbili, Kairuki alisema Kinondoni imekutwa na watumishi hewa 107 na kama wangelipwa ingepoteza Sh bilioni 1.279 na kwa Halmashauri ya Kishapu waligundulika 73 na wangelipwa Sh milioni 543.
Kairuki alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Maida Hamad Abdallah (CCM) aliyetaka kujua hasara serikali imeipata kwa kuwalipa watumishi hewa na adhabu kwa waliohusika na suala hilo.
Alisema, “Hadi sasa watumishi hewa 19,629 wamebainika na kama wangelipwa, kwa mwezi wangeingiza hasara ya Sh 19,749,737,180. Kuhusu adhabu na kurejesha fedha, Kairuki alisema mahakama imekuwa ikitekeleza majukumu yake na kuwatoza faini na wengine kutakiwa kurejesha fedha.
Awali, akijibu swali la msingi la Abdallah aliyetaka kujua serikali inasema nini juu ya wale wote waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo ya watumishi hewa, huku waliohusika wengi wakiwa ni maofisa na watumishi wa serikali, Kairuki alisema hadi Oktoba 25 mwaka huu serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi 1,663.
Kairuki alisema watumishi hao ni kutoka katika wizara, idara zinazojitegemea, wakala wa serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ambao walibainika kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa na 638 kati yao wamefunguliwa mashitaka polisi.
Akitoa mchanganuo, Kairuki alisema idadi ya watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu katika wizara ni 16, idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali ni tisa, Sekretarieti za mikoa sita na Mamlaka ya Serikali za Mitaa 1,632 wanaofanya idadi ya watumishi 1,663 waliochukuliwa hatua.
“Hatua hii inajumuisha kuwasilishwa kwa masuala yanayowahusu baadhi ya watumishi hawa katika vyombo na ulinzi na usalama na hadi kufikia tarehe 25.10.2016, watumishi 638 mashitaka yako polisi, 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na watumishi 975 mashtaka yao yamefikishwa kwenye mamlaka zao za kinidhamu,” alisema Kairuki.
Alisema sambamba na hatua hiyo, serikali inaendesha ukaguzi wa mara kwa mara wa Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (HCMIS) na maofisa wanaobainika kuhusika au kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika taasisi na mamlaka zao, huchukuliwa hatua za kinidhamu, kama vile kuwafungia dhamana na uwezo wa kuingia na kufanya kazi katika mfumo huo.