ASKARI Polisi wa Mkoa wa Songwe, Sasi Mwita na mkewe Pendo Mwita wamekufa katika ajali iliyotokea Dodoma. Watoto wao watatu wamejeruhiwa katika jali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Seruka kata ya Chipogolo Wilaya ya Mpwapwa, katika barabara kuu ya Dodoma – Iringa.
Ajali hiyo pia imesababisha kifo cha askari wengine wa mkoa wa Songwe, PC Mahende na Emmaculata Nyangi.

Katika ajali hiyo, gari yenye namba za usajili T.517 CDL Toyota Alphard iliyokuwa ikiendeshwa na Aggrey Lucas (27) mkazi wa Dar es Salaam, iliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 10.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Ernest Kimola, waliokufa kwenye ajali hiyo ni F.7142 PC Sasi Mwita na H.8816 PC Mahende wote wa Polisi Songwe, Pendo Mwita (mke wa askari PC Sasi Mwita) na Emmaculata Nyangi.
Amewataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Neema Mwita (8), Judy Mwita (4) Jenifa Mwita (4) Nyangi Wambura (23), F286 PC Nashon wa Polisi Tunduma, Baraka Chacha (9), F.8667 PC Enock (mmiliki wa gari).
Wengine ni Nyakonyoro Charles, Elizabeth na Enock Jeremia.
Alisema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma na wanapatiwa matibabu.
Aidha alisema chanzo cha ajali ni kutokana na mwendokasi na kusababisha dereva kushindwa kumudu gari na kusababisha ajali hiyo.