TUME ya Mufti imetoa siku saba kwa wote wanaohodhi mali mbalimbali zikiwemo magari na pikipiki vilivyosajiliwa kwa jina la Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), kuviwasilisha kwa ajili ya uhakiki na watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo, watachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Tume ya Mufti, Shehe Abubakari Khalid, alisema jana kuwa tume yake katika utekelezaji wa hadidu za rejea za majukumu yake, inawataka wale wote wanaohodhi vyombo vya moto vilivyosajiliwa kwa jina la Bakwata katika mkoa wa Dar es Salaam, waviwasilishe kwa ajili ya uhakiki katika Ofisi za Bakwata makao makuu barabara ya Kinondoni, Dar es Salaam, kuanzia Desemba 14, mwaka huu.
“ Wale walioko mikoani waviwasilishe kwa uhakiki katika Ofisi za Bakwata mikoa husika, pia makatibu wa mikoa watekeleze ndani ya muda huo maagizo waliopewa kuhusiana na kadhia hiyo,” alisema Shehe Khalid.
Alisema baada ya siku saba kupita Bakwata kwa kushirikiana na mamlaka husika, litaendesha msako mkali na kuchukua hatua za kisheria kwa wale ambao hawatatekeleza agizo hilo.
Aliongeza kuwa tume hiyo, inawashukuru wale wote wanaoendelea kutoa ushirikiano na kuipa tume hiyo taarifa muhimu zinazohusu mali za Bakwata, zinazomilikiwa kinyume cha sheria na kuwataka waendelee kufanya hivyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata taifa na mjumbe wa Tume ya Mufti, Shehe Khamis Mataka alisema kumekuwa na suala la taasisi za dini kupata misamaha kwenye kodi na uhakiki huo una lengo la kupata idadi ya magari na pikipiki yaliyopata msamaha nchi nzima.
“Uhakiki huo pia utasaidia kujua idadi ya magari yaliyopo na hali zake kwani kuna mengine yamekwisha na hayatumiki tena ni vizuri kufanya uhakiki,” alisema Mataka.
Pia alisema uhakiki huo, baadae utahamia kwenye mali nyingine za baraza hilo, ikiwemo nyumba na viwanja.
“Ndio maana leo tupo Dodoma kufanya kazi tuliyopewa na Mufti na Baraza linataka kujiridhisha idadi ya vyombo vya moto vilivyopo nchi nzima itasaidia kujua vipo wapi na vina hali gani. Alisema uhakiki wa mali za baraza nchi nzima unafanyika kutokana na utaratibu wa tume hiyo kukusanya taarifa ambayo ripoti ya kwanza tayari ilishawasilishwa kwa Mufti.