Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama
SERIKALI imesema Ukimwi bado ni janga kubwa nchini na kwamba kwa mujibu wa takwimu, maambukizi kwa Tanzania Bara ni asilimia 5.6, huku waathirika wakubwa wakitajwa kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, vijana na wanawake.
Aidha, wakati ikiadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani nchini jana, serikali imezindua Mfuko wa Udhamini wa ugonjwa huo pamoja na Bodi yake.

Mfuko huo utawawezesha Watanzania kuchangia janga hilo ili kupatikana uwezo wa ndani katika kupatikana dawa na huduma nyingine.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2015, watoto chini ya miaka mitano na vijana ndiyo waathirika wakubwa wa ugonjwa huo, kama ilivyo kwa kundi la wanawake lililoathirika zaidi kwa asilimia 6.2 ikikinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 3.8.
Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama ambaye katika taarifa yake alisema Ukimwi bado ni janga kubwa nchini na kwamba kwa mujibu wa takwimu maambukizi kwa Tanzania Bara ni asilimia 5.6.
“Katika kila Watanzania 100, Watanzania watano wana maambukizi ya Ukimwi, katika kila wanawake 100 Tanzania, wanawake sita wana maambukizi na katika kila wanaume 100 nchini, wanaume wanne wana VVU,” alisema Jenista jana wakati Tanzania ikiuungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.
Alisema inakadiriwa kuwa watu 1,538,382 wanaishi na maambukizi ya ugonjwa huo huku vijana umri wa miaka 15 hadi 24 wakiwa ni asilimia 10.6 na watoto chini ya miaka mitano wakiwa asilimia 11.8.
Aidha, alisema asilimia 50 pekee ndio wanaopata dawa za kufubaza virusi wa ugonjwa huo na kwa mujibu wa, takwimu za mwaka juzi, maambukizi mapya ni watu 48,000 kwa mwaka.
Alisema katika mkakati wa kupambana na ugonjwa huo, dunia imejiwekea lengo kutokomeza ugonjwa huu kuwa kama janga ifikapo 2030 na kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS), limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90).
Aidha, serikali iliwahimiza wananchi kuendelea kujitokeza kupima afya zao ili wajitambue na kujua namna ya kujilinda na kuchukua hatua za kujikinga na maambukizi ya VVU, kwani jitihada kubwa zimefanyika za kuwaelimisha kuhusu ugonjwa huo.
Alisema maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yanazitaka nchi kuwaanzishia dawa mara moja watu wote watakaopima na kugundulika wana vvu yaani “Test and Treat”.
Wizara ya Afya imeshatoa waraka wa kuanza mpango huu tangu Oktoba mwaka huu.
Alisema mpango huo unatarajiwa kuongeza mahitaji ya huduma za matibabu na dawa kwa sababu badala ya kuwa wanaotakiwa kupata dawa za kupunguza makali ni wale wenye CD4 count chini ya 500, sasa itakuwa yeyote atakayepima na kukutwa na VVU anatakiwa kuanzishiwa dawa mara moja.
“Hili si jambo dogo. Linahitaji rasilimali za kutosha hasa rasilimali za ndani hivyo, ninapongeza jitihada zilizofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu/TACAIDS za kuanzisha Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (AIDS Trust Fund). Hatua hii ni muhimu sana kwa nchi yetu katika kutimiza wajibu tulionao wa kutoa huduma za tiba kwa waathirika wa VVU,” alieleza.
Kuhusu mfuko huo, aliwaomba Watanzania kujitokeza kuuchangia ili kuwa na uwezo kama nchi wa rasilimali za kutosha dhidi ya Ukimwi zinazotokana na mapato ya ndani.