Baraza la dini lenye ushawishi mkubwa nchini Somalia limesema kuwa michuano ya kitaifa ya mpira wa kikapu miongoni mwa wanawake ambao unaanza Alhamisi nchini humo inakiuka maadili ya Kiislamu, kulingana na mtandao wa kibinafsi wa Jowhar.

Ni mashindano ya kwanza ya mpira wa kikapu miongoni mwa wanawake nchini Somalia, huku timu kutoka majimbo yote matano pamoja na mji mkuu wa Mogadishu zikishiriki.
Lakini mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Bashir Ahmed Salat amenukuliwa akisema mashindano hayo yanaenda kinyume na utamaduni wa kiislamu.
''Tunaonya kuhusu michezo ya wanawake ,ni kitu ambacho Uislamu unapinga.Sio vizuri kwa wanaume kuwaona wanawake wamevalia sare za michezo kidini na pia kitamaduni''.
Baraza hilo linasimamiwa na viongozi wa dini wenye msimamo wa wastani na wanalipinga kundi la wapiganaji wa al-Shabab ambalo limeweka sheria kali kuhusu tabia za wanawake mbali na mavazi yao katika maeneo linalodhibiti.
Mapema mwaka huu, baraza hilo lilikosoa mswada kuhusu haki za wanawake ambao serikali inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa uliuchukua na kuufanyia marekebisho .
Mechi ya kwanza ya mpira wa vikapu inaanza mji wa kaskazini mashariki wa Garowe, ambapo kutakuwa na mechi kati ya Hirshabelle na Mogadishu.