SERIKALI na taasisi mbalimbali zimeombwa kuwapatia elimu walemavu wasioona wa kituo cha Matembe Bora kilichopo Buigiri, wilaya ya Chamwino ili waweze kuboresha kilimo chao bustani za mboga.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kituo hicho, Yared Chileso kwa niaba ya wenzake wakati walipokuwa wakipokea msaada wa vifaa mbalimbali, zikiwemo nguo, sabuni, viatu na mafuta ya kupakaa vilivyotolewa na Umoja wa madhehebu ya Kikristo mkoa wa Dodoma.

Chileso alisema kuwa kutokana na wao kujishughulisha na ukulima wa mboga kwa lengo la kutaka kujiinua kiuchumi wameomba kupatiwa wataalamu hao ili waweze kuwapatia elimu itakayowawezesha kuboreshewa na hatimaye kuongeza kipato na kujiinua kiuchumi.
“Sisi tuliopo hapa kituoni ni walemavu wa macho wasioona lakini pamoja na ulemavu huo tunajishughulisha na kilimo cha mboga kama vile mchicha, kabichi, nyanya, spinachi na pilipili za kawaida na hoho, lakini hatuna utaalamu hivyo tunaomba wataalamu ili watuwezesha kwa kutupatia elimu zaidi ya kilimo,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa kupitia kilimo hicho cha mboga wameweza kupata fedha za kusomesha watoto wao na matibabu.
Aidha mwenyekiti huyo alisema kupatiwa kwa wataalamu hao kutawezesha kuachana na tabia ya ombaomba ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi ya watu wasiojiweza, kwa kuwa tayari tutakuwa tumeonesha mfano kwa vituo vingine vinavyotunza watu wenye mahitaji maalumu.