SERIKALI imeziagiza halmashauri kuzifanyia ukaguzi jumuiya za maji zilizoanzishwa kisheria katika maeneo yao, ili kubaini ubadhirifu wa fedha kwa kuwa unaweza kusababisha miradi ya maji isiwe endelevu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa jana mjini hapa, katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.

Amesema viongozi wa jumuiya za maji katika halmashauri wamezigeuza kuwa “serikali ndogo” wakifanya wanavyotaka, hivyo kuhatarisha ustawi wa miradi ya maji.
Waziri Lwenge amesema, jumuiya nyingi za maji hazijafungua akaunti benki, fedha zinazochangishwa na watumiaji wa maji katika maeneo yao zinahifadhiwa na viongozi wake ambao wanazitafuna wanavyotaka.
Amezitaka halmashauri nchini kuhakikisha kuwa jumuiya za maji zinaazishwa kwa kufuata sheria ya maji ya mwaka 2009 katika miradi yote ya maji iliyoanzishwa vijijini ili kuifanya iwe endelevu.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven alimweleza Waziri Lwenge kuwa mkoa huo unakadiriwa kuwa na idadi ya wakazi 1,154,760, ambapo upatikanaji wa maji safi na salama ni asilimia 50.2 kupitia mtandao wa miradi 234 iliyopo mkoani humo.