Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kwa sasa Tanzania haina tatizo la njaa, isipokuwa kuna upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo na endapo kungekuwa na baa hilo la njaa, mwenye mamlaka ya kulitangaza tatizo hilo ni mkuu wa nchi pekee na si watu wengine.
Aidha, kimewataka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini, kuacha kutumia matatizo yanayowakumba wananchi kwa maslahi yao ya kisiasa na kufanya uchochezi, badala yake watumie fursa walizonazo kutafuta suluhu ya matatizo hayo.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa hali ya siasa nchini.
Polepole alisema wakati CCM ikishughulikia matatizo ya wananchi kwa viongozi wake kupitia Serikali ya Awamu ya Tano, kutekeleza na kusimamia sera na Ilani ya CCM ya mwaka 2015/20, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiirudisha nyuma serikali hiyo kwa kuendeleza siasa chafu zenye mrengo wa kuwachan ganya na kuwarubuni wananchi.
“Ndio maana nasema CCM inatekeleza mfumo wa siasa safi na uongozi bora na mara zote hatupendi malumbano yasiyo na tija. Wapo baadhi ya wanasiasa na viongozi wa upande wa pili, wanaotumia fursa hii ya upungufu wa chakula kwa kueneza uzushi na uongo kwa wananchi kuwa kuna baa la njaa,” alisema.
Polepole aliwataka Watanzania wawapuuze viongozi kama hao, kwani hawana nia njema na taifa zaidi ya kueneza uchochezi na kuwashtua wananchi kwa lengo la kuifanya serikali iliyo chini ya chama tawala cha CCM kuwa imeshindwa.
Alisema kwa muda sasa kumekuwa na mazungumzo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa (si CCM) wanaodai kuwa nchi inakabiliwa na njaa na kufafanua kuwa duniani kote upo utaratibu wa kufuatwa unaotumiwa na nchi zote duniani ukiwemo Umoja wa Mataifa (UN) endapo nchi ina njaa unaotangazwa rasmi la mkuu wa nchi.
Alifafanua kuwa kwa muda wa miaka 30 sasa Tanzania haijawahi kukumbwa na tatizo lolote la njaa kutokana na ukweli kuwa serikali zote zilizopita, zilijitahidi kuhamasisha wananchi kufanya kazi na kukabiliana na ukame pale ulipotokea.
Alisema kama ilivyo miaka mingine, ambayo nayo ilikumbana na tatizo la ukame, mwaka huu nao katika baadhi ya maeneo kumekuwa na ukame na upungufu wa chakula, lakini sio baa la njaa kama inavyodaiwa.
“Kipindi hiki tulichonacho bado hatujafika huko kwenye njaa, ilikuwa matarajio yangu kuwa kunapotokea tatizo la upungufu wa chakula kama hili viongozi wote pasipo kujali utofauti wa itikadi na vyama, tungehamasisha watanzania wafanye kazi kwa bidii, wahifadhi chakula na wasitengenezee nafaka pombe. Jamani hili ni jukumu letu sote si CCM wala serikali pekee,” alisisitiza.
Alisema chama hicho kimebaini kuwa wapo viongozi ambao hawana hata taarifa za kutosha kuhusu suala hilo la chakula, lakini wanatumia fursa hiyo kueneza propaganda zao za kisiasa kwa maslahi yao.
“Naomba niwakumbushe kutoa taarifa za uongo zitakazoamsha taharuki miongoni mwa wananchi ni kosa la jinai. Zipo mamlaka zinazoweza kutoa vyema ufafanuzi kuhusu jambo hili. Nashukuru tayari serikali imeanza kufafanua na kubainisha hatua zinazochukuliwa kukabili hali hii,” alisisitiza.
Alisema amesikitishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa walioibuka hivi karibuni na kudai nchi ina baa njaa na kubainisha bado serikali haijafahamu malengo yao nini.
“Yupo mwingine ametokea naye na kudai kuwa eti atawaombea chakula Watanzania na kuwagawia bure. Hivi taifa litaendeleaje endapo litakuwa na wananchi wasiofanya kazi wanaosubiri chakula bure? Naombeni Watanzania viongozi wa aina hii tuwapuuze,” alisema.
Alisema CCM imekuwa daima ikifanya siasa zake kwa kuzingatia ukweli hivyo endapo kungekuwa na njaa kweli, chama hicho kingesema ukweli kwani sera yake ni kusema ukweli, fitina kwake ni mwiko. “Hizi fitina tunawaachia wao,” alisema.
Alisema viongozi wanaotumia matatizo ya wananchi kwa maslahi yao, wanaonesha wazi kuwa hawafuati nyayo za CCM za kufanya siasa safi na uongozi huku akitolea mfano baadhi ya wanasiasa walivyotumia tatizo la tetemeko mkoani Kagera kueneza siasa chafu kwa maslahi yao.
Pamoja na CCM kutoa kauli hiyo, juzi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa ufafanuzi suala hilo la upungufu wa chakula na kubainisha kuwa serikali itasambaza kiasi cha tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji ili kupunguza ongezeko la bei.
Waziri Majaliwa alibainisha kuwa katika msimu uliopita, kulikuwa na tani milioni tatu za chakula, lakini baada ya shinikizo la wananchi tani milioni 1.5 ziliuzwa nje na kubakisha tani milioni 1.5. Aidha, kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kulikuwa na akiba ya mahindi tani 88.152.