KESI ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili, Salum Njwete ‘Scorpion’, imeahirishwa hadi Januari 25 mwaka huu kutokana na shahidi ambaye ni daktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuwa nje ya kituo hicho.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga alidai katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba walipanga kumleta shahidi huyo wa nne katika kesi hiyo.

Alidai shahidi huyo ndiye aliyemhudumia Said Mrisho na alitarajiwa kufika mahakamani hapo jana lakini alipata dharura kwa kuwa yupo nje ya kituo chake cha kazi.
“Shahidi huyu ambaye tumemtegemea ameshindwa kuja leo (jana) kutokana na dharura. Tulipowasiliana naye alisema dharura hiyo inaisha baada ya wiki tatu,” alidai Katuga.
Pia alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 225 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), inataka kesi ihairishwe kwa wiki mbili endapo mshitakiwa atakuwa mahabusu hivyo aliomba mahakama ipange tarehe ya katikati ili ihairishwe na kupangwa tarehe ya kusikiliza.
Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alikubaliana na ombi hilo kwamba hana pingamizi. Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 25 mwaka huu itakapotajwa.