![]() | |
|
MAMIA ya wananchi wamejitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani huku ulinzi ukiimarishwa katika vituo vya kupiga kura 29.
Ofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jamilla Mahenga alisema kazi hiyo imefanyika vizuri katika vituo vyote huku wananchi wakipiga kura kwa utulivu wa hali ya juu.
“Tumefungua vituo vya kupiga kura mapema asubuhi na watu wamejitokeza kwa wingi na matokeo yatatangazwa mara baada ya kukamilisha mchakato wa kuhesabu kura,” alieleza Mahenga.
Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juma Ali Juma alipiga kura yake katika kituo cha Shule ya Sekondari ya Fuoni, ambako baada ya kupiga kura alizungumza na waandishi wa habari na kuelezea matumaini yake makubwa ya kuibuka na ushindi wa kishindo.
“Sina wasiwasi hata kidogo hili ni jimbo la CCM tangu awali kwa hivyo nitaibuka na ushindi mkubwa wa kishindo dhidi ya wapinzani wangu ikiwemo chama cha CUF,” alieleza mgombea huyo wa CCM.
Akizungumza baada ya kumaliza ukaguzi wa vituo mbalimbali, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu HamidMahmoud alisema amefurahishwa na maandalizi ya uchaguzi huo ambao umetoa nafasi na fursa kubwa kwa wapiga kura kushiriki kikamilifu katika shughuli hiyo ya kidemokrasia.
“Nmekagua zaidi ya vituo sita vya Uchaguzi Mdogo Jimbo la Dimani na kuridhishwa na maandalizi ya wapiga kura walishiriki katika zoezi hilo kwa fursa kubwa bila ya malalamiko,”
alieleza.
alieleza.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alisema ulinzi imeimarishwa zaidi katika baadhi ya vituo baada ya kuwepo kwa taarifa za fujo na vurugu.
“Tumeimarisha ulinzi wa baadhi ya maeneo baada ya kupata taarifa kwamba upo uwezekano wa kuibuka kwa vurugu za uchaguzi...sehemu unapowaona wapo Polisi wengi maana yake zipo fununu za kuwepo vurugu,” alieleza Mahmoud.
Mkazi wa Bweleo, Ali Issa alisema amepiga kura yake mapema saa mbili mara baada ya kuanza mchakato wa kupiga kura na kurudi nyumba mara baada ya kumaliza kazi hiyo na kuendelea na shughuli zake.
“Nilipeleka shahada yangu niliyopiga kura katika uchaguzi wa marudio mwaka juzi na ikahakikiwa tayari kupiga kura ya uchaguzi mdogo,” alieleza Issa.
Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ali Tahir kilichotolea huo Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge, Novemba mwaka jana.
Aidha, uchaguzi huo umekwenda sanjali na Uchaguzi Mdogo katika wa Madiwani kata 20 za Tanzania Bara ambazo hazikuwa na madiwani kwa sababu mbalimbali.

0 Comments