Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Malinyi, Marcelin Ndimbwa
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Marcelin Ndimbwa amewapongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kutokana na ushindi wa kishindo wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani uliofanyika karibuni.

Pongezi za Ndimbwa kwa Rais Magufuli na Kinana, zimekuja siku chache baada ya CCM kuibuka na ushindi huo katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Dimani, Zanzibar na udiwani kwenye kata 19 kati ya 20 Tanzania Bara.
Mkurugenzi Ndimbwa ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) Mkoa wa Morogoro, alilazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 350 kutoka Malinyi hadi Morogoro Mjini ili kuwaongezea nguvu wanaCCM wa Morogoro Mjini wakiongozwa na Mkurugenzi wake John Mgalula, hatua iliyoleta hamasa na kufanikisha ushindi huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Ndimbwa alisema ushindi huo wa kwanza tangu Rais Magufuli apokee kijiti cha uenyekiti wa CCM Taifa kutoka kwa mtangulizi wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, umetoa salamu za kishindo kwa wapinzani.
“Hizi ni salamu tosha, nimeona ni vema nimpongeze sana Mwenyekiti wetu (Magufuli) lakini pia Katibu wetu (Kinana) kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kukijenga chama na hasa mpango thabiti wa kuirejesha CCM kwa wananchi masikini kama ilivyokuwa dhimira ya kuanzishwa kwake, “Ushindi wa CCM ni uthibitisho wa wazi kuwa uongozi wa serikali ya awamu ya tano, upo kwa ajili ya watu na matatizo yao, na ni ishara kuwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa serikali hii, imani ya wananchi kwa CCM imeimarika zaidi ya ilivyokuwa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” alisema.
Alisema pamoja na pongezi hizo, wanaCCM wanaoshikilia nafasi mbalimbali za uongozi serikalini wachukulie ushindi wa CCM kama chachu ya kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao ili kuendelea kuongeza imani ya wananchi kwa chama na serikali yao.
Alisema ni kwa kulitambua hilo ndio maana serikali wilayani Malinyi imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kasi, ikiwemo kuboresha miradi ya afya, elimu, miundombinu, kilimo na kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi.
CCM mbali ya kushinda kiti cha ubunge cha Dimani visiwani Zanzibar, imeshinda kata 19 kati ya kata 20 zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani juzi kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kufa kwa waliokuwa wakishikilia nyadhifa hizo na kufutwa kwa matokeo kwa amri ya Mahakama.
Kata ambazo CCM imeshinda ni Nyarenanyuki (Arumeru, Arusha), Isegehe (Kahama, Shinyanga), Nkome (Geita), Kiwanja cha Ndege (Manispaa Morogoro), Lembeni (Mwanga, Kilimanjaro), Ihumwa (Dodoma), Matevez (Meru, Arusha) na Kimwani (Muleba, Kagera).
Pia Igombavanu (Iringa), Ikwea (Iringa), Kijichi (Mbagala, Dar es Salaam), Ng’hambi (Dodoma), Kinampundu (Singida), Kasansa (Katavi), Malya na Kahumulo (Mwanza), Mkoma (Mara), Misugusugu (Kibaha, Pwani). Aidha CCM ilishindwa katika Kata moja tu ya Duru mkoani Manyara, ambako mgombea wa Chadema aliibuka mshindi.