KAMPUNI ya Reli Tanzania (TRL) imetaja baadhi ya sababu zilizosaidia kusiwepo na matukio ya vifo katika tukio la ajali ya treni ya abiria ya Deluxe, iliyotokea juzi katika kijiji cha Kikongo Mlandizi wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.
Miongoni mwa sababu zilizofanya abiria wote kupona ni kutokana na dereva kuwa kwenye mwendo wa kawaida; hivyo kuwezesha mabehewa ambayo yaliacha reli kutopandana, kama ilivyowahi kutokea kwa ajali nyingine.
Kaimu Mkuu wa Usalama wa Reli wa TRL, Marko Gukwi aliliambia gazeti hili jana kuwa sababu nyingine iliyosaidia ni kuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya dereva anayekaa mbele na mwangalizi wa treni ambaye anakaa nyuma.
Alisema mwangalizi wa treni, ndiye aliyeona mabehewa yanaanza kuacha njia, hivyo akakanyaga breki kwa haraka kama njia ya kumtaka dereva kusimamisha treni. “Guard alisaidia kwa kiasi kikubwa yasitokee madhara makubwa, kwani alimpa ishara ya haraka dereva wake naye akatii na kusimama haraka,” alieleza Gukwi.
Gukwi ambaye alikuwa anazungumza na gazeti hili eneo la tukio, aliongeza kuwa jambo lingine ambalo lilisaidia kusiwepo na madhara makubwa ni kutokana na treni hiyo kuwa na mabehewa ambayo ni imara.
Alisema mabehewa hayo yametengenezwa nchini Korea. Alisisitiza kuwa uongozi wa TRL uko makini na roho za watu na akawaomba wananchi waichukulie ajali hiyo kuwa ya kawaida, kama ilivyo kwa ajali nyingine.
“Tunashukuru kwamba madhara sio makubwa na hii inatokana na kampuni kuhakikisha kuwa treni zake zinazosafiri zinakuwa salama na kukaguliwa kila wakati,” aliongeza.
Katika ajali hiyo, watu watano walijeruhiwa, mmoja akiwa ana hali mbaya na hivyo kuwahishwa katika Hospitali ya Tumbi baada ya mabehewa tisa ya treni ya abiria ya Deluxe iliyokuwa ikitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kuanguka.
Katika mabehewa hayo, manne yameanguka, matatu yameacha njia na mawili yametenguka. Uchunguzi kufanyika Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Focus Sahani ambaye alikuwepo eneo la tukio tangu juzi jioni, alisema hadi jana walikuwa hawajafahamu kilichosababisha ajali hiyo, hivyo wataalamu wa shirika hilo wanachunguza kubaini chanzo chake.
“Kipaumbele chetu kwa sasa ni kuhakikisha kwamba njia inafunguliwa kwanza, ndipo uchunguzi na mambo mengine yatafuata hapo baadaye,” alisema Sahani.
Aliongeza katika kuhakikisha kwamba njia hiyo inafunguliwa kufikia jana saa 9 alasiri, walipeleka mafundi wapatao 164 katika eneo hilo la ajali. Gazeti hili lilishuhudia mafundi wa TRL wakiwasili kutoka Dar es Salaam na Morogoro juzi kuanzia saa 7 za usiku wakiwa na vifaa vyote vinavyohitajika katika matengenezo ya reli hiyo. Vifaa hivyo ni reli, mataruma, winchi la kunyanyulia mabehewa yaliyoanguka na injini za kuvuta mabehewa yaliyokuwa yameacha reli.
“Sisi wafanyakazi wa TRL na vyombo vingine vya serikali tuko hapa kuhakikisha kwamba kufikia saa 9 alasiri leo, njia inafunguliwa tena na ndio maana unaona tuna timu kubwa ya watu ambao wanaendelea kufanya ukarabati,” alisema Sahani.
Reli ambako ajali hiyo imetokea iliharibika kwa kiasi kikubwa ikiwemo kung’oka katika baadhi ya sehemu na katika maeneo mengine reli ilijipinda, jambo ambalo lilifanya mafundi waondoe reli hiyo na kuweka reli nyingine.
Hatua nyingine muhimu ambayo ilifanywa na mafundi hao jana ni kuhakikisha wanayaondoa eneo la tukio mabehewa matatu, ambayo yaliacha njia ili waweze kufanya matengenezo ya reli kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Sahani, mabehewa hayo lazima yawekwe kwenye reli na yaondolewe eneo hilo ili ujenzi wa reli uendelee. Naibu Mkurugenzi huyo alisema wafanyakazi walikuwa na nguvu na ari ya juu, kuhakikisha kwamba wanafanya matengenezo hayo katika kipindi walichokubaliana.
“Tumeshawasiliana na Dar es Salaam kwamba gari ya abiria kwenda Bara ambayo ilishindwa kuondoka jana (juzi) wairuhusu iondoke saa 9.00 alasiri,” aliongeza.
Alisema njia ikishafunguliwa na kuanza kupitika, ndio juhudi za kuinua mabehewa mengine matano ambayo yalikuwa yameanguka kabisa na kuacha reli yataanza kunyanyuliwa kwa kuwa tayari vifaa vyote viko katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa hilo likishakamilika, ndipo sasa timu ya kuchunguza chanzo cha ajali itaanza kufanya kazi yake ili kubaini tatizo lilikuwa ni nini hadi kusababisha treni kuanguka.
“Ni lazima tuchunguze maana ajali ilitokea wakati kichwa na mabehewa mengine yameshapita, lakini behewa la 11 ndilo lilianza kuanguka, lazima tubaini chanzo,” alibainisha.
Alisema mabehewa yaliyoanguka, pia hayakuharibika hivyo yatapelekwa kwenye karakana za kampuni hiyo na matengenezo yake yanaweza kuchukua kama miezi miwili tu.
Alikiri kuwa katika kipindi ambacho watakuwa wanafanya matengenezo kutakuwa na upungufu wa mabehewa kwa treni hiyo ya Express.
Reli imechakaa Mhandisi Mkuu Ujenzi wa TRL, Nelson Ntejo alisema kwamba ili kuhakikisha kwamba kazi inafanyika kwa haraka, alilazimika kuchukua mafundi wote ambao walikuwa wanafanya ukarabati wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Pugu na wengine kutoka Morogoro.
“Vifaa tumepokea kutoka Dar es Salaam na Morogoro ndio maana unaona kazi inafanyika kwa haraka,” alisema Ntejo ambaye alisema kwamba suala la uangalizi wa miundombinu ya reli ya Kati liko kwa shirika hodhi la reli yaani RAHCO.
Alisema wanaotakiwa kuifanyia matengenezo reli hiyo ni RAHCO kwani TRL wenyewe ni watumiaji tu wa miundombinu hiyo.
Lakini alisema kwa kuwa wanajali usalama wamekuwa wanalazimika kufanya matengenezo madogo madogo katika reli hiyo.
Alikiri kuwa reli hiyo imechakaa na ndio maana RAHCO wana mpango wa kuibadilisha kutoka reli ya ukubwa wa paundi 60 inayotumika sasa hadi kuwa paundi 80.
Alisema mradi huo utaanza kujengwa Februari mwaka huu na unahusisha ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Isaka.
“Pamoja na kwamba mimi sio msemaji wa RAHCO, lakini tunavyofahamu ni kwamba mradi huu umeshatengewa fedha kiasi cha dola za marekani milioni 300,” alieleza.
Njia yafunguliwa Jana jioni, TRL ilitoa taarifa kwamba kuanzia saa 9 alasiri njia ya reli kati ya Kituo Kikuu cha Dar es Salaam na Ruvu imefunguliwa rasmi kwa shughuli za uendeshaji wa reli.
Taarifa hiyo ilisema kazi ya ufunguaji njia imewezekana baada ya wahandisi na mafundi wa reli kuyaondoa mabehewa yaliyopata ajali kutoka relini na pia kuikarabati sehemu iliyoharibika.
Kazi hiyo imefanyika kuanzia usiku wa Januari 29, 2017 hadi mchana wa jana. Aidha, treni ya abiria iliyoahirisha safari ya kuondoka kwenda Bara jana, imeondoka leo saa 9:05 alasiri kutoka Kituo Kikuu cha Dar es Salaam kwenda Bara.
Wakati huo huo, imefahamika kuwa msafiri mmoja, Basekena O. Bango kutoka Bujumbura nchini Burundi akiwa anasafiri kutoka Kigoma, amelazwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani wa Pwani kwa ajili ya matibabu zaidi. Aligunduliwa kuwa amechanika mguu wake wa kulia hivyo basi kuhitaji kushonwa mguu wake huo.
Taarifa kutoka Muhimbili zinaeleza kulazwa kwa majeruhi wawili, waliopokewa hospitalini hapo juzi usiku.
Majeruhi hao ni Stephania Mbona (46) kutoka Kigoma aliyekuwa anakwenda Muhimbili, kuendelea na matibabu ya ugonjwa wa tumbo, hata hivyo alitibiwa majeraha ya kawaida na anaendelea kulazwa kwa ajili ya matibabu ya tumbo.
Mgonjwa mwingine, Alice Jovin (37) mkazi wa Salasala Dar es Salaam alikuwa anatoka Kigoma, amepata majeraha ya kawaida ametibiwa na alitarajiwa kuruhusiwa jana asubuhi. Kuhusu idadi ya wasafiri treni ya Deluxe yenye uwezo wa kusafirisha abiria zaidi ya 1,000, TRL imesema wakati inapata ajali ilikuwa na abiria 480.
“Aidha, imefahamika kuwa ili kufahamika hasara na sababu za ajali hiyo taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi wa kamati maalumu inayoundwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji reli za kimataifa. Taarifa hiyo itatolewa baada ya wiki mbili,” ilieleza taarifa ya TRL.
|
0 Comments