Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jan 3, 2017

Shein aahidi makubwa Kiwanda cha kutengeneza matrekta Mbweni

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukiendeleza Kiwanda cha Matrekta Mbweni.
Alisema hiyo inatokana na umuhimu wa kiwanda hicho katika kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na sekta nyingine za ufundi visiwani humo.

Dk Shein aliyasema hayo jana baada ya kufanya ziara katika kiwanda hicho akiwa amefuata na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi pamoja na watendaji wakuu wa Serikali wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk Abdulhamid Yahaya Mzee.
Katika maelezo yake Dk Shein alisema kuwa ziara hiyo aliyoifanya akiwa na viongozi wengine wa Baraza la Mapinduzi na Watendaji Wakuu wa Serikali ni ushauri wake wa kuwataka viongozi hao washiriki pamoja wapate kujua muelekeo, hatma, nyenzo, wafanyakazi, mambo yanayohitajika pamoja na changamoto zilizopo.
Akiwa katika ziara yake hiyo ya kwanza ya kikazi kwa mwaka huu 2017, Dk Shein alisema kuwa tokea kuanzishwa kiwanda hicho mnamo mwaka 1966 hakijapiga hatua kubwa licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali kwa ushirikiano ya Serikali ya China na baadae mnamo mwaka 1980 Serikali ya Uholanzi kuziunga mkono ikiwemo kukijengea uwezo wa kiufundi na kiutawala.
Dk Shein alisema kazi ya kikiendeleza Kiwanda hicho si ndogo lakini akimnukuu shujaa wa Ufaransa Napoleon Bonaparte, aliyekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1799 alivyosema kuwa “Tulikwenda, Tukaona na Tukashinda”, basi anaamini mafanikio yatapatikana baada ya ziara hiyo.
“Tumekuja, tumeona na tutashinda lakini kubwa ni mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali na wafanyakazi wa Kiwanda hichi... tujiandae kubwa lijalo”, alisema Dk Shein.
Hata hiyo, Dk Shein alisisitiza haja ya kutofanya kazi kwa mazoea kwa kuutaka uongozi na wafanyakazi wa kiwanda hicho kuyaweka vizuri mazingira ya kiwanda pamoja na kuviweka vifaa vichakavu katika utaratibu maalum ambapo licha ya changamoto zilizopo lakini Kiwanda hicho kinaweza kuvutia iwapo hatua hizo zitachukuliwa.
Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed alitoa shukrani za pekee kwa Rais Shein kwa ziara yake hiyo ya mara ya pili katika kiwanda hicho na kueleza jinsi anavyofanya uamuzi kwa ushirikiano kati yake na wasaidizi wake na hakurupuki katika hilo.
Nao wafanyakazi wa Kiwanda hicho katika risala yao iliyosomwa na Mkuu wa Kitengo cha zana za Kilimo, Mohammed Omar Mohammed walisema kuwa wanajivunia ujio wa Rais kwa mara ya pili katika kipindi cha takriban miaka mitatu kwa lengo la kujali kazi ambazo Karakana hiyo inazitekeleza.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP