Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jan 3, 2017

Sijaitelekeza Kagera -JPM


Rais John Magufuli akizungumza na Wakazi wa Muleba mkoani Kagera mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili mkoani humo jana. (Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli amefafanua hatua alizochukua baada ya kutokea tetemeko mkoani Kagera ikiwa ni pamoja na kuahirisha safari yake ya kikazi nje ya nchi na kuteua mawaziri sita akiwemo Waziri Mkuu kwa ajili ya kufuatilia hali ilivyo mkoani humo.
Aidha, Rais huyo amebainisha wazi kuwa serikali haitoweza kumjengea nyumba kila muathirika wa tetemeko hilo na badala yake itajikita zaidi katika kuboresha huduma muhimu kwa jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya na nishati.

Dk Magufuli alisema hayo, wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Ishozi, wilayani Misenyi mkoani Kagera jana ambako pia aliweka jiwe la msingi kwenye Kituo cha Afya kinachojengwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Ninafahamu mwaka jana kulitokea tetemeko, baada ya kupata taarifa nilimtuma waziri mkuu na mawaziri karibu sita, pia niliahirisha ziara ya siku tatu kwenda nchini Zambia,” alisisitiza Magufuli.
Mara baada ya kupatikana kwa taarifa za tetemeko hilo, lililosababisha vifo vya takribani watu 17 na kuharibu mali ikiwemo nyumba, Rais huyo alikuwa anatarajiwa kwenda Lusaka Zambia kwa ziara ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine angehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Sita wa nchi hiyo Edgar Chagwa Lungu.
Nyumba za waathirika
Akizungumzia maafa hayo ya tetemeko, aliwataka wakazi wa mkoa huo kutambua kuwa kamwe serikali haiwezi kuwajengea waathirika wa tetemeko hilo kila mmoja nyumba.
“Najua kuna baadhi ya wanasiasa waliokuwa wanawapotosha wananchi kwa kuwaambia kuwa serikali itawajengea nyumba waathirika. Hili halina ukweli. Kwani hata nchi zilizoendelea kama vile Italia na Japan hazijawahi kuwajengea waathirika wa matetemeko nyumba,” alisisitiza.
Alisisitiza kuwa serikali haina kiasi hicho cha fedha kuweza kuwajengea wananchi hao nyumba na kuwataka wakazi wa mkoa huo kuwajibika na kila mmoja kujenga nyumba yake.
Kamati za Maafa
Aidha Dk Magufuli alibainisha kuwa muda wa kamati ya maafa ya Kagera iliyopo chini ya Mkuu wa Mkoa wa miezi mitano ni mwingi, hivyo umefika wakati wa kamati hiyo kuvunjwa na badala yake mkoa huo uanze sasa kuwekeza nguvu zake kwenye shughuli za maendeleo.
“Hata ikifanyika harusi, kamati ya harusi inapomaliza muda wake huvunjwa, hivyo hivyo ukitokea msiba, kamati yakusimamia shughuli za msiba nayo ukiisha huvunjwa. Na hii nayo tena sasa ina miezi mitano na inawezekana wajumbe wanaendelea kulipana posho, nayo ivunjwe,” alisisitiza.
Alisema baada ya kamati hiyo ya mkoa kuvunjwa, kamati ya Maafa iliyopo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo Dar es Salaam, ihamie mkoani Kagera kwa ajili ya kusimamia michango ya maafa inavyokwenda.
Aidha, aliagiza kamati hiyo ya taifa ya maafa kuhakikisha inatumia fedha zilizotolewa na wadau mbalimbali kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani humo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Fedha za Maafa
Rais huyo alibainisha kuwa fedha zote za maafa zilizokusanywa ziliwasilishwa mkoani humo kwa ajili ya kupangiwa shughuli za kukabiliana na maafa hayo na kwamba Sh bilioni sita zilizotolewa na serikali ya Uingereza kwa ajili ya maafa hayo, zilitumika kujengea shule ya Uhungo, itakayojengwa kisasa.
Hata hivyo, alisema anatambua kuwa takribani Sh bilioni 4.5 zilizoahidiwa bado hazijawasilishwa na waliotoa ahadi.
“sitaki kuwataja wahusika ila nawafahamu naomba waziwasilishe hizo fedha,” Uwajibikaji Katika hotuba hiyo Dk Magufuli aliwataka viongozi wa mkoa wa Kagera kutambua kuwa sasa janga hilo la maafa limeisha na iliyobaki ni muda wa kuwajibika na kujenga maendeleo ya mkoa huo. “Kwa sasa haya maafa yameisha, naomba viongozi wa mkoa huu akiwemo RC muwasimamie wananchi wachape kazi, ni wakati wa kuijenga Kagera mpya na muwe mfano,” alisema Rais Magufuli.
Msaada wa chakula
Pamoja na hayo, Dk Magufuli alisisitiza kuwa serikali haina mpango wa kugawa chakula cha msaaada kwa wakazi wa mkoa huo wa Kagera kwa kuwa mkoa huo ni kati ya baadhi ya mikoa nchini iliyobarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba.
Aliwataka viongozi wa mkoa huo akiwemo Mkuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya kusimamia wananchi wao ili waweze kuwajibika ipasavyo.
“Kila mtu lazima afanye kazi kwa bidii, acheni kuzurura zurura hovyo,” Awali, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali Dennis Mwila, wakati akitoa taarifa ya wilaya hiyo mbele ya Rais, alisema kati ya kata 20 zilizopo wilayani humo, kata nne zinakabiliwa na tatizo kubwa la njaa hivyo zinahitaji msaada wa chakula.
Kufutwa Kodi
Pamoja na hayo Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk Charles Tizeba kuhakikisha anafuta utitiri wa kodi zote za hovyo, wanazotozwa wakulima ili kuwapunguzia mzigo wakulima hao.
Alisema amebaini kuwa katika zao pekee la kahawa lina jumla ya utitiri wa kodi takribani 30 jambo linalowabebesha mzigo wakulima na kushindwa kunufaika na mazao yao. Alisema kutokana na tatizo hilo la utitiri wa kodi katika mazao, zao la kahawa linalolimwa pia nchini Uganda, lina bei nzuri sokoni ikilinganishwa na kahawa inayolipwa Tanzania.
“Kodi nyingine zinashangaza, hakuna anayewanunulia dawa, au kuwalipia pembejeo hawa wakulima sasa mnawatoza kodi zote hizi za nini hebu zifuteni,” alisisitiza na kuongeza kuwa endapo Ma-RC, Ma-DC na Ma-DED wanafikiri kodi ni chache sana za kilimo na wao waende wajaribu kulima ili waone shida wanayopata wakulima.
Elimu
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametangaza rasmi kuibadilishia umiliki shule ya sekondari Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Chama cha Mapinduzi _Wazazi na kuanzia sasa shule hiyo itamilikiwa na Serikali.
Kutokana na agizo hilo, Dk Magufuli alimtaka Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kufuatilia maendeleo ya fedha zilizotumika katika kuikarabati shule hiyo.
Alipoitembelea shule hiyo jana asubuhi, alitaarifiwa kuwa hadi sasa ukarabati wa shule hiyo umegharimu kiasi cha Sh milioni 110 wakati kwa mujibu wa ripoti aliyonayo, inaonyesha jumla ya Sh milioni 172 zimeshatumika katika ukarabati huo.
Miundombinu
Halikadhalika, Rais Magufuli pia aliwahakikishia wakazi wa kanda ya ziwa kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara na Shinyanga kuwa serikali iko kwenye mchakato wa kununua meli kubwa kwa ajili ya kutumika kwenye Ziwa Victoria ili kupunguza adha ya usafiri.
Akizungumza na wananchi katika shule ya sekondari ya Ihungo, jana alisema mchakato huo unaendelea ambapo zitanunuliwa meli mbili zitakazotumika katika ziwa hilo Victoria na Ziwa na Tanganyika.
“Ninaelewa kuwa wakazi wa Kagera wanakabiliwa na tatizo la usafiri tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996, nawaahidi kwa kipindi cha muda mfupi ujao tatizo hili litakuwa ni historia. Aidha alisema pamoja na kwamba tayari serikali imenunua ndege mbili, inaendelea na mchakato wa kukamilisha ununuzi wa ndege nne zaidi zikiwemo kubwa za kisasa ili kukamilisha mpango wake wa kununua ndege sita. “Nimepanga kuwa Rais wa wanyonge, Rais atakayelikomboa taifa hili haiwezekani watu milioni 52 tusiwe na ndege hata moja, halafu eti taifa lenye watu milioni 10 liwe na ndege. Ndege za kisasa ambazo tutazileta mwaka kesho hakuna shirika lingine la ndege Afrika ambalo limeleta ndege kama hizo,” alisisitiza.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP