|
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza thamani ya mazao yake kabla ya kuyauza nje ya nchi.
Alisema kwa muda mrefu serikali ilikuwa inapata hasara kwa kusafirisha malighafi nje ya nchi, lakini kwa sasa inajenga viwanda ili iweze kuuza bidhaa.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati alikizungumza na wakulima wa chai katika kijiji cha Lwangu wilayani Njombe.
“Miaka mingi serikali imekuwa ikipata hasara kwa kuuza mazao nje ya nchi, tumeamua kujenga viwanda vitakavyoweza kuyachakata na kuuza bidhaa badala ya malighafi. Ujenzi wa viwanda ni moja kati ya mikakati dhati ya serikali ya kuhakikisha mazao mnayolima yanakuwa na thamani kubwa hivyo kuwaongezea tija,” alisema Majaliwa.
Aliwataka wananchi kuongeza juhudi katika kilimo.
“Kuna anayetaka hela hapa? Kama mnataka mali mtazipata shambani. Limeni,” alieleza.
Alisema mazao hayo ndiyo yatakayoweza kuleta tija kwa wakulima, hivyo aliwashauri waendelee kushirikiana katika vikundi ili wapate misaada ya kitaalamu kwa urahisi.
Aidha, alimuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Ruth Msafiri na maofisa kilimo kuwatembelea wakulima hao kwa lengo la kuwaelekeza namna bora ya kuendeleza mazao yao.
Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli, alisema kilimo cha chai ndio mkombozi kwa wananchi hao, hivyo aliwaomba waongeze juhudi.
Awali, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kutoa Huduma kwa Wakulima Wadogo Njombe (NOSC), Filber Kavia, alisema kampuni hiyo inatoa huduma za kitaalamu kwa wakulima.
Alisema wanalenga kuendeleza kilimo cha chai kwa kuongeza kuongeza uzalishaji kwa hao kutoka kilo 500 hadi kilo 2,000 za majani makavu ya chai kwa hekta kwa mwaka.
Alisema kampuni hiyo inakusudia kuongeza mashamba mapya ya chai hadi kufikia hekta 3,800 kutoka hekta 614 ifikapo mwaka 2025.
0 Comments