ASILIMIA 58 ya wanawake na 40 ya wanaume, wanakubali kwamba ni sahihi kwa mume kumpiga mke wake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo akiunguza chakula.
Hayo yamebainika katika matokeo ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania kwa mwaka 2015/2016 (TDHSMIS), uliogusa maeneo mbalimbali ya maisha yanayohusu afya ya uzazi, malezi na athari za malaria nchini.

Aidha wamekubali kwamba ni sahihi mume kumpiga mke wake endapo atabishana naye, atakwenda mahali bila kumuambia, hatawajali watoto au atakataa kushirikiana naye tendo la ndoa.
Utafiti huo umefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara na Wizara ya Afya kwa Zanzibar.
Meneja wa Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Sylvia Meku alisema kwamba asilimia 48 ya wanawake na wanaume asilimia 31 wakati wa utafiti huo, walikubali kuwa ni sahihi mume kumpiga mke wake endapo hatowajali watoto.
Alisema utafiti huo ulishirikisha sampuli wakilishi ya kitaifa iliyohusisha wanawake 13,266 wenye miaka 15-49 katika kaya zote zilizochaguliwa, na wanaume 3,514 wenye miaka 15-49 katika theluthi ya kaya zilizochaguliwa kuingia katika sampuli walifanyiwa mahojiano.
“Idadi hii inawakilisha mwitikio wa asilimia 97 kwa wanawake na asilimia 92 kwa wanaume. Sampuli ya utafiti huu inaruhusu kufanyika kwa makadirio kwa Tanzania nzima, maeneo ya mijini na vijijini, Tanzania Bara na Zanzibar na kwa Kanda kama zinavyotumiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto” alisema Meku akielezea utafiti huo hivi karibuni.
Alisema kwa upande wa ukatili wa kimwili, wanawake wanne kati ya 10 wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili tangu wakiwa na umri wa miaka 15 na kati mwaka mmoja uliopita wanawake wawili kati ya 10 walikumbana na ukatili wa kimwili.
“Ukatili wa kimwili unaongezeka kadri umri unavyoongezeka ambapo asilimia 22 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 wamewahi kukumbana na ukatili wa kimwili ikilinganishwa na asilimia 48 ya wanawake wenye umri wa miaka 40-49,” alisema.
Meku alisema kimkoa, kiwango cha ukatili wa kimwili kipo kati ya asilimia sita katika mkoa wa Kusini Pemba mpaka asilimia 61 katika mkoa wa Mara.
Alisema kiwango cha vitendo vya ukatili wa kimwili ni kikubwa miongoni mwa wanawake ambao wametalikiwa, wameachika au wajane ambayo ni asilimia 63 ikilinganishwa na wanawake walioolewa au ambao hawajawahi kuolewa ambao ni asilimia 16.
“Watuhumiwa wakubwa wa unyanyasaji wa kimwili miongoni mwa wanawake waliowahi kuolewa au kuishi na wenza ni mume au mwenza wa sasa kwa asilimia 63. Miongoni mwa wanawake ambao hawajawahi kuolewa, vitendo vya ukatili wa kimwili walivyofanyiwa, vilifanywa na mwalimu kwa asilimia 23,” alisema.
Kwa upande wa ukatili unaohusisha ngono, asilimia 17 ya wanawake wamewahi kufanyiwa vitendo vya ukatili vinavyohusisha ngono, ambapo asilimia tisa wamepata unyanyasaji unaohusisha vitendo vya ngono katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
“Vitendo vya ukatili unaohusisha ngono vinaongezeka kulingana na umri, kuanzia asilimia nane kwa wanawake wenye umri wa miaka 15- 19 hadi asilimia 18 kwa wanawake wenye umri wa miaka 40-49,” alisema.
Meku alisema vitendo vya unyanyasaji unaohusisha vitendo vya ngono, vipo zaidi katika mkoa wa Shinyanga ambao ni asilimia 33. Akizungumzia ukatili katika kipindi cha ujauzito alisema, asilimia nane ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 ambao wamewahi kuwa wajawazito, wamewahi kukumbana na vitendo vya ukatili wakati wa ujauzito.
Alisema vitendo vya ukatili wakati mama ni mjamzito vinaweza kutishia hali ya mama mjamzito na pia hata mtoto anayetarajiwa kuzaliwa. Kuhusu ukatili baina ya wenza, utafiti huo umeonesha kwamba asilimia 42 ya wanawake waliowahi kuolewa, wamewahi kukumbana na ukatili wa wenza wao, ama kimwili au ukatili unaohusisha ngono.
Alisema kwa kila wanawake 10, wanawake watatu walisema kuwa waliwahi kufanyiwa vitendo vya ukatili na wenza wao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Alisema kiwango cha vitendo vya ukatili kutoka kwa wenza, kiko juu miongoni mwa wanawake ambao wanaume au wenza wao hawana elimu ambao ni asilimia 53 au walevi wa mara kwa mara kwa aslimia 74 na kwa wale ambao baba zao walikuwa wakiwapiga mama zao kwa asilimia 54.
Hata hivyo, Meku alisema zaidi ya nusu ya wanawake ambao wamewahi kukumbana na vitendo vya ukatili wa kimwili au wa kingono, walitafuta msaada ili kukomesha vitendo hivyo.
Alisema wanawake hao wengi wao walitumia njia ya kuomba msaada kwa wanafamilia wao ambao ni asilimia 56 na kwa familia ya mume au mwenza wake ambao ni asilimia 42.
Utafiti huo ulizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambapo alisema matokeo hayo yataisaidia serikali na wadau wengine katika kutathmini na kufuatilia utekeleza wa mipango endelevu katika huduma za afya nchini.