Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameendelea kuing’ang’ania Kampuni ya TANCOAL Energy, inayochimba makaa ya mawe kwenye Mgodi wa Ngaka, kwa kusema kuwa kwa mujibu wa mkataba, ilitakiwa iwe imeshaanza kuzalisha umeme, lakini hadi leo haijaanza.
Kwa mujibu wa mkataba, mbali ya kuzalisha makaa ya mawe, kampuni hiyo ilipaswa kuzalisha umeme wa megawati 400 kutokana na makaa hayo. TANCOAL ina migodi miwili ambayo ni Mbalawala na Mbuyura ambao umetengwa mahsusi kwa ajili ya kuzalisha umeme.

“Kwenye mkataba tulikubaliana kuwa mtazalisha umeme, lakini hadi leo hamjaanza mnadai kuwa TANESCO wanawachelewesha. Nitafuatilia nione kama ni wao au la ili tujue ukweli,” alisema Waziri Mkuu mara alipotembelea na kukagua uzalishaji katika mgodi huo.
Waziri Mkuu aliitaka kampuni hiyo ya TANCOAL Energy itimize masharti ya mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008. Kampuni ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources Limited, ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation East Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited, ambayo hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa.
Mgodi wa Ngaka uko wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na unamilikiwa na kampuni ya TANCOAL kwa ubia baina ya NDC na kampuni ya Intra Energy Corporation ya Australia. Kwa mujibu wa mkataba huo, TANCOAL ilipaswa kugharamia Dola za Marekani milioni 14.49 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ili kuwezesha malori makubwa na madogo yaweze kufika mgodini na kusomba makaa hayo.
“Mlisema mngetengeneza barabara lakini hadi sasa bado hamjafanya hivyo na ndiyo maana malori yanaishia kule. Yangefika hapa moja kwa moja, mngeweza kubaini kwa urahisi mahitaji ya makaa ya mawe ni kiasi gani,” alisema Waziri Mkuu.
Hivi sasa, malori kutoka mgodini yanashusha makaa yaliyochimbwa kwenye eneo lililokodishwa na TANCOAL la Amani Makolo, ambalo liko umbali wa kilometa 55 kutoka mgodini. Malori makubwa yanapakia makaa hayo kutoka kwenye eneo hilo, jambo ambalo linazidisha gharama za usafirishaji.
Kwa mujibu wa mkataba huo, TANCOAL ilipaswa kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 82, lakini hadi sasa imewekeza kiasi cha dola milioni 14 ambazo ni sawa na asilimia 12 tu ya ahadi iliyotolewa.
“Makubaliano yalikuwa ninyi mtawekeza Dola za Marekani milioni 81.69 lakini hadi sasa mmetumia dola za Marekani milioni 14, hamjafikia hata nusu,” alisema Waziri Mkuu. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk. Samuel Nyantahe afuatilie kwa makini mambo yanayoendelea ndani ya shirika hilo.